Habari Mseto

Yaibuka Sharon Otieno alisema na Gavana Obado mara 6

September 7th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

KISA cha kutatanisha cha mauaji ya kinyama ya mwanachuo Sharon Otieno kinazidi kupata sura mpya, huku sasa mwanga ukizidi kupatikana kuhusu tuhuma kuwa huenda kulikuwa na mkono wa mwanasiasa mashuhuri kutoka eneo la Nyanza katika mauaji hayo.

Runinga ya K24 kiliripoti Alhamisi kuwa siku ya mauaji ya mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Rongo ambaye maiti yake ilipatikana Jumatano asubuhi, Bi Otieno walizungumza na Gavana wa Migori Okoth Obado mara sita.

Aidha, kituo hicho kiliripoti kuwa mwendazake alimtumia Gavana Obado ujumbe mfupi saa mbili usiku Jumatatu, muda mfupi baada ya mwanahabari Barrack Oduor ambaye walitekwa nyara naye kujiokoa kutoka mikononi mwa watekaji nyara, akimuuliza kwanini mambo yalikuwa yakimwendea kombo.

“Siku ya kutekwa nyara kwa Sharon Otieno na mwanahabari Barrack Oduor, Sharon alizungumza na Gavana Obado mara sita, ishara kwamba walikuwa na uhusiano wa karibu au hata (Gavana Obado) alimfahamu mwendazake,” kituo hicho kikatangaza.

“Cha kustaajabisha ni kwamba siku aliyotekwa nyara Sharon alimtumia gavana huyo ujumbe mfupi mwendo wa saa mbili jioni akitaka kujua ni kwanini mambo yalionekana kumwendea mrama.”

Kulingana na kituo hicho, maafisa wa upelelezi sasa wamekata kauri kumhoji Gavana Obado, kwa nia ya kubaini ukweli ikiwa alihusika.

“Maafisa wa upelelezi wamefichua kuwa watamhoji Gavana wa Migori Okoth Obado ili kubaini ikiwa alihusika na mauaji ya mwanadada huyo ambaye alikuwa mja mzito,” kikasema kituo hicho.

Wakati huohuo maombolezi na simanzi zinaendelea kutawala nyumbani kwa mwendazake katika kaunti ya Migori, kufuatia mauaji ya kinyama kwa mwanao, kwa kile kinachokisiwa kuwa mzozo uliokuwa wa kimapenzi.

Viongozi mbalimbali wakiongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga pamoja na Wakenya wengi wametaka uchunguzi wa mauaji hayo kuharakishwa na haki kutolewa kwa familia hiyo.

Jumanne, wanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo waliandamana wakitaka kuelekea nyumbani kwa Gavana Obado, lakini maafisa wa kuzuia ghasia wakawa wameshika doria.

Tangu mauaji hayo kutendeka, bado Gavana Obado hajajitokeza waziwazi kuzungumzia suala hilo, ingawa mkuu wa mawasiliano katika afisi yake Nicholas Anyuor amekuwa akilizungumzia, akisema ni maadui wa gavana huyo wanaotaka kumharibia sifa.