Siasa

Yaibuka vijana waliotumika kupanga ghasia za Kenol waliahidiwa Sh500

October 6th, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

VIJANA waliotumiwa na wanasiasa wa mirengo ya Tangatanga na Kieleweke mjini Kenol, Kaunti ya Murang’a Jumapili iliyopita walikuwa wameahidiwa kulipwa kati ya Sh500 na Sh1,000, wapelelezi wameambia Taifa Leo Dijitali.

Imeibuka kuwa wengi wa vijana hao si wakazi wa kaunti hiyo, na walitolewa kaunti za Nairobi na Kiambu kuzua vurugu katika makabiliano yaliyowaacha watu wawili wamefariki.

Polisi wamethibitisha kuwa gavana mmoja, wawakilishi wawili wanawake na mbunge mmoja, wote kutoka eneo la Mlima Kenya walifadhili safari za mabasi yaliyowapeleka vijana hao kwenye kuzua ghasia.

Kwenye mpango huo mchafu pia alikuwepo mbunge mmoja kutoka jijini Nairobi aliyewalipia vijana hao gharama zote. Wanasiasa wa upande wa Kieleweke walipanga njama za kuhakikisha kuwa masafara wa Naibu Rais kuelekea Kenol umekwazwa huku wale wa Tangatanga pia wakilipa vijana kupangua njama zote za kumzuia Dkt Ruto.

Kundi moja la kisiasa lililipa vijana kutoka mitaa ya Wetethie na Kiandutu mjini Thika huku kundi pinzani likisafirisha vijana kutoka mitaa ya Mwiki, Githurai, Kasarani, Kayole na hata Kibera.

Hoteli tatu, moja mjini Maragua, nyingine mjini Thika na ya tatu katika eneo la barabara ya Thika zilitumika kuandaa mipango ya vurumai na kushawishi vijana tangu Jumatano.