Habari Mseto

Yaibuka wakazi hulisha mifugo ndani ya mbuga ya Tsavo

March 6th, 2019 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

WAFUGAJI waliovamia kaunti ya Taita Taveta, wamebuni mbinu mpya ya kulisha mifugo wao ndani ya mbuga ya Tsavo.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa maelfu ya mifugo wanalishwa katika mbuga ya Tsavo usiku, huku maafisa wa shirika la wanyama pori KWS wakidai kutojua kinachoendelea.

Walishaji hao haramu huingiza mifugo hao usiku kupitia mianya iliyo chini ya reli ya SGR katika maeneo ya Maungu, Miasenyi na Makina.

Wenyeji waliambia Taifa Leo kuwa maelfu ya mifugo huingizwa katika mbuga ya Tsavo Mashariki kila siku kuanzia mwendo wa saa kumi na mbili hadi saa moja usiku.

Mifugo hao hutolewa alfajiri kufichwa katika ranchi zinazopakana na hifadhi hiyoili kusubiri kurejreshwa nbuygani usiku.

“Mimi huona mifugo hao kila siku. Wafugaji hao hugawa mifugo kwa makundi ya ng’ombe 150-200,” akasema Bi Jane Matano mwenyeji wa Miasenyi.

Bi Matano alieleza kuwa wakazi wa eneo hilo hawaruhusiwi kulisha mifugo mbugani.

Hata hivyo, Msimamizi wa eneo la Tsavo, Bw George Osuri alisema hana habari kuhusu suala hilo hili akiahidi kuchunguza yeye binafsi.

Bw Osuri alisema kuwa njia za reli hulindwa na maafisa wa KWS ili kuzuia wahalifu kuingia mbugani.