Habari Mseto

Yaibuka Wakenya tayari washakopa Sh6.2 bilioni kwa Fuliza

February 8th, 2019 2 min read

VICTOR JUMA na BENSON MATHEKA

WATEJA wa kampuni ya Safaricom walikopa Sh6.2 bilioni kupitia huduma mpya ya kukopa pesa ya Fuliza katika kipindi cha mwezi mmoja pekee, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw Bob Collymore amefichua.

Bw Collymore alisema wateja 4.2 milioni wamekopa pesa kupitia huduma hiyo ambayo ni ushirikiano wa Safaricom na benki za Commercial Bank of Africa (CBA) na Kenya Commercial (KCB). Kupitia huduma ya Fuliza, Wakenya hukopeshwa pesa za kulipa mikopo ya Mshwari na KCB Mpesa.

Riba huwa ni asilimia 1.083 kwa siku, kwa pesa zinazokopwa. “Idadi ya wateja ambao wanatumia huduma hii (Fuliza) ni 4.2 milioni na Sh6.2 bilioni zimekopwa,” Bw Collymore aliambia gazeti la Business Daily.

Hii inamaanisha kwamba kila siku wateja wa Safaricom hukopa zaidi ya Sh200 milioni kupitia huduma ya Fuliza kiwango ambacho kinazidi cha baadhi ya benki ndogo nchini. Wateja wanaweza kukopa hadi Sh70,000  kulingana na jinsi wanavyotumia huduma ya M-Pesa na wanavyolipa madeni yao.

Huduma ya Fuliza inalenga watu walio na mahitaji ya dharura ya pesa hasa kulipa bili za matibabu, kodi ya nyumba na hata washirika wao wa kibiashara.

“Kwa mteja, kuchelewa kulipa ni kukosa nafasi muhimu sana au biashara.Tunaamini hii ndiyo sababu Fuliza imekuwa maarufu,mno miongoni mwa wateja wetu,” alisema Bw Collymore.

Alisema kampuni ilianzisha huduma ya Fuliza ili kusaidia wateja kulipa madeni yao kwa wakati. Ikijumuishwa, riba ya asilimia 1.083 kwa siku ni ya juu mno ikiwa ni sawa na asilimia 395.2 kwa mwaka.

Benki hutoza riba ya asilimia 13 kwa mwaka ikiwa ni asilimia 0.035 kwa siku. Hata hivyo, wateja wengi huamua kutumia huduma za kutoa mikopo kwa simu au mtandao kwa sababu zinachukua muda mfupi na masharti ni nafuu.

Kutokana na idadi kubwa ya Wakenya wanaohitaji mikopo mashirika mengi yamechipuka kama vile Letshego, Tala, Branch, Izwe na Mycredit. Mashirika haya hutoa mikopo inayopaswa kulipwa kwa muda wa kati ya siku moja na mwezi mmoja.