Makala

Yalikuwa makosa kuunganisha polisi wa utawala na wa kawaida – Wadadisi

March 7th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

WADADISI wa masuala ya usalama sasa wanaungama kwamba hatua ya Septemba 13, 2018, ya kuunganisha polisi wa utawala (AP) na wenzao wa majukumu ya kawaida ndio kiini cha kudorora kwa usalama katika maeneo mengi nchini.

Kupitia pendekezo la Katiba Mpya ya 2010 ambayo iliunda kikosi kimoja cha polisi chini ya amri ya Huduma ya Polisi Nchini (NPS), AP waliunganishwa na wenzao wa kawaida na kwa pamoja, wakaanza kufahamika kama kikosi kimoja.

Mtaalamu wa masuala ya utawala tangu enzi za uhuru wa nchi Bw Joseph Kaguthi, anasema kwamba hatua hiyo ya vikosi hivyo kuunganishwa haikuwa ya busara.

“Vitengo hivyo vilikuwa na utofauti na upekee mkubwa sana katika huduma. Kikosi cha AP kilikuwa na majukumu ya utawala huku hiki kingine kikiwa kizuri katika operesheni mbalimbali. Kwa sasa huo mpangilio umesambaratika,” anasema Bw Kaguthi.

Alisema AP walikuwa wakitangamana kwa undani na wananchi mashinani na kujenga ule umoja wa mashauriano kati ya serikali na raia, kiasi kwamba habari muhimu zilikuwa zinawafikia maafisa kabla ya hali kuwa tete.

“Binafsi ninahisi ule ushirikiano wa raia na polisi umepungua na spidi ya serikali kupashwa habari kwa wakati ufaao imepungua,” anasema, akiongeza kwamba hiyo ndio sababu ya machafuko kutokea katika maeneo mbalimbali nchini kabla ya serikali kujipanga.

Mwenyekiti wa muungano wa polisi wastaafu Mlima Kenya Cyrus Mugambi, anasema kwamba hakuwa na busara yoyote kuunganisha vitengo hivyo viwili.

“Wakati machifu walikuwa na maafisa wa polisi wa utawala katika kambi zao kulikuwa na afueni la kiusalama. Kwa kuwa machifu ni wazaliwa na wakazi wa maeneo yao ya huduma, kulikuwa na ule udharura wa kuwajibikia visa vya uhalifu Kwa wakati ufaao,” anasema Bw Mugambi.

Anaongeza kwamba kulikuwa na ule ushindani wa kitengo gani ndicho cha kuibuka na matokeo bora zaidi na wananchi wakawa ndio washindi.

“Serikali ya Rais Mwai Kibaki ilitambua nafasi ya maafisa wa AP katika kusaidia kutawala nchi na hata katika machafuko ya kisiasa ya baada ya uchaguzi wa 2007, AP walitumika kwa kiwango kikuu kudhibiti uharibifu katika miji mikuu kama ya Nairobi, Kisumu na Mombasa,” anasema.

Lakini wadadidi wanasema shida ilitokea wakati serikali ya Kibaki ilionyesha mapenzi yake ya dhati ‘kupindukia’ kwa maafisa wa AP kwa kuwa iliwasaidia kuwaboreshea mazingira ya kikazi na muda kidogo kukazuka visa vya vitengo vingine kuhisi kutengwa.

“Maafisa wa AP walianza kupata vifaa bora, kupandishwa ngazi haraka upesi, kuwa na urafiki mkuu na serikali kupitia utawala wa mikoa na hata kuwa na mianya mingi ya kuhudumu katika majukumu ya kupata pesa,” akasema.

Uhasama huo unasemwa kwamba uliingia katika utayarishaji wa rasimu iliyozaa Katiba Mpya ambapo wengi wa maafisa wakuu wa polisi wa kawaida waliungana na wakapinga harakati za kitengo hicho cha AP kutambuliwa kama asasi kivyake.

Kwa mujibu wa Waziri wa Masuala ya Umma Moses Kuria, “kulitokea pendekezo kwamba kuwe na Inspekta Mkuu wa Polisi wa kila kitengo lakini wakubwa wa polisi wa kawaida wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Nairobi King’ori Mwangi walikataa”.

Anasema kwamba ilipendekezwa vikosi hivyo viwili viunganishwe ili kuleta umoja wa kikazi ndani ya polisi na pia kuzima visa vya ushindani ambao ulikuwa ukikanganya kazi ya polisi kiasi cha kuzua uasi.

Huku maafisa wa kawaida wakiwa ndio walikuwa na uwezo wa kuwazuilia washukiwa na kuwashtaki mahakamani, ulifika wakati kwamba maafisa wa utawala wakitia washukiwa mbaroni, polisi wa kawaida walikuwa wakikataa kuwaweka kwa seli au kuwashtaki.

Hali haikusaidiwa na hatua ya serikali kuwapa maafisa wa AP uwezo wa kuwa na vitabu vya matukio (OB) vya kuwasajili rasmi washukiwa kwa kuwa hatimaye walikuwa wakihitajika kuwawasilisha washukiwa hao katika vituo vya polisi chini ya usimamizi wa maafisa wa kawaida.

Hali tata zaidi ilikuwa kwamba Kamanda wa Kituo cha Polisi (OCS) ndiye aliyekuwa wa kuidhinisha uamuzi wa kushtaki washukiwa.

Uhasama uliotokea ukawa kwamba mara kwa mara washukiwa wakikamatwa na AP, walikuwa wakiachiliwa huru.

Wakati serikali ilianza kusaidia AP kupata uwezo wa kushtaki washukiwa ndipo taswira ya hatari ilianza kujiangazia baina ya vitengo hivyo viwili.

Ni hali ambayo hata Naibu Rais Rigathi Gachagua amejiunga na mjadala kuihusu, akiungama kwamba “kuna tetesi halali kwamba vitengo hivyo viwili vilikuwa na huduma spesheli kwa kila kimojawapo”.

Akihutubia washirikishi wa masuala ya usalama eneo la Pwani kuhusu janga la mihadarati na ulevi, Bw Gachagua alisema vituo vya polisi viko mbali na watu na maafisa wa AP walikuwa karibu na raia.

“Ule urafiki wa AP na raia ulikuwa unatusaidia katika upangaji wa mikakati. Bila kujiingiza kwa undani katika mjadala huu, ni wazi kwamba vitengo hivyo viwili vilikuwa vinatufaa vikiwa jinsi vilivyokuwa,” akasema Bw Gachagua.

[email protected]