Habari MsetoSiasa

Yaliyojadiliwa Ruto alipofanya kikao cha siri shambani mwake Taveta

January 11th, 2020 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

NAIBU Rais William Ruto ameanzisha mikakati ya kuwinda kura katika eneo la Taita Taveta ili ‘kunyakua’ kaunti hiyo ambayo kwa sasa ni ngome ya chama cha ODM.

Mnamo Alhamisi, Bw Ruto alifanya mkutano wa faragha katika shamba lake la Mata, katika eneo la Taveta.

Mkutano huo ulijumuisha viongozi wa Jubilee na wawaniaji wa chama hicho katika kaunti hiyo.

Kikao hicho ambacho kilikuwa kimepangwa na mbunge mwakilishi wa wanawake, Bi Lydia Haika na yule wa Taveta Dkt Naomi Shaban kilijadili maswala mbalimbali yakiwemo uchaguzi wa chama unaokuja na vilevile mwelekeo wa chama hicho katika eneo hilo.

Duru za kuaminika zilieleza kuwa, Bw Ruto aliomba viongozi hao kuunga mkono azma yake ya kutwaa urais na kuwaahidi mabadiliko ikiwa atachukua mamlaka 2022.

Alisema chama cha Jubilee kiko imara na wala hakitatikiswa na watu kutoka nje ambao wanapanga njama ya kukiangamiza.

Alisema wale wanaovuruga Jubilee si wanachama na, wala hawajawahi kuunga mkono chama hicho.

“Jubilee ni chama cha kitaifa na kiko imara. Hatutaruhusu watu ambao si wanachama kuzua vurugu katika chama chetu,” akasema.

Vilevile, naibu Rais alitangaza msimamo wake wa kuunga mkono ripoti ya BBI licha ya kauli zake za hapo awali ambapo amekuwa akiipinga.

Bw Ruto alisema ataunga mkono ripoti hiyo ila tu lazima mapendekezo yake yapitishwe na wananchi.

“Hatutaki swala la watu fulani kufanya maamuzi ya kujipendekeza wao. Lazima Wakenya wapewe nafasi ya kujiamulia wao wenyewe,” akasema.

Bi Haika aliambia Taifa Leo kuwa, mkutano huo ulinuia kufanya maandalizi ya uchaguzi wa chama unaokuja mnamo Machi mwaka huu.

Mbunge huyo hata hivyo alikiri kuwa wameweka mikakati ya kuvumisha azma ya naibu Rais katika eneo la Pwani ili kutafuta uungwaji mkono katika ukanda huo.

Alisema tayari chama hicho kitaanza kuandaa mikutano ya viongozi na makundi mbalimbali katika kaunti ya Taita Taveta.