Yaliyojiri kabla ya Gicheru kuaga dunia

Yaliyojiri kabla ya Gicheru kuaga dunia

NA VINCENT ACHUKA

RIPOTI mpya zimeibuka kuhusu nyakati za mwisho za wakili aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Paul Gicheru aliyepatikana akiwa amefariki kwenye makazi yake mnamo Jumatatu usiku.

Imebainika kuwa mwendazake aliyefariki akiwa na umri wa miaka 52, alitumia dakika zake za mwisho akinywa divai nyumbani kwake Karen, kabla ya mke wake kumpata akiwa amezimia pamoja na mwanawe.

Bw Gicheru alikuwa anasubiri ICC kutoa uamuzi wake kuhusiana na iwapo aliwahonga mashahidi waliostahili kutoa ushahidi katika kesi dhidi ya Rais William Ruto iliyotupiliwa mbali miaka sita iliyopita.

Alitangazwa kufariki dunia muda mfupi baada ya saa moja usiku Jumatatu katika hospitali ya Karen alipokuwa amekimbizwa kutibiwa.

Iliarifiwa kuwa marehemu hakuwa anaugua maradhi yoyote na ilikuwa nadra kwake kutoka nje ya nyumba yake nambari tisa kwenye mtaa wa kifahari wa Northwood Villas, Miotoni Lane, Karen, ambapo kodi ya chini kabisa ya nyumba kila mwezi ni Sh400,000 tangu alipohamia eneo hilo miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa wafanyakazi wake waliozungumza kwa faragha na Taifa Leo, siku ya kifo chake, mwendazake alikuwa nyumbani kwake pamoja na mke wake Ruth, mwanawe, Allan, 22, baba mkwe wake Wangombe Wokabi pamoja na mjakazi wake mmoja kwa jina Dorcas.

Wafanyakazi hao walisema kuwa bosi wao alishinda mchana kutwa Jumatatu katika chumba chake binafsi kilicho kwenye ghorofa ya juu ya nyumba yake yenye vyumba vitatu akibugia divai aliyopenda.

Alishuka chini tu mwendo wa saa kumi jioni kuomba maji kisha akarudi juu.

“Mke wake na baba mkwe walikuwepo lakini alishinda mchana kutwa chumbani kwake na alishuka mara moja tu,” mmoja wa wafanyakazi wake alieleza Taifa Leo jana Jumanne.

Hakukuwa na kitu chochote kilichoonekana kuwa si cha kawaida hadi muda mfupi baada ya saa moja usiku wakati mke wake alipanda juu kuuliza ikiwa Gicheru angejiunga nao kula chajio ambapo alimpata akitokwa povu mdomoni.

Alipoenda katika chumba kilichokuwa karibu, Bi Gicheru alimpata mwanawe akiwa amepoteza fahamu.

Ambulensi iliitwa mara moja kuwakimbiza hospitalini Bw Gicheru na Alan ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Uingereza.

Bi Gicheru na mjakazi wao mmoja, Dorcas, pia waliingia ndani ya ambulensi kumpeleka wakili na mwanawe hospitalini.Dorcas alirejea na habari za kuhuzunisha kuwa wakili huyo alitangazwa kufariki saa nne usiku Jumatatu.

  • Tags

You can share this post!

Mpira wa Vikapu: Timu nne za Kenya zawinda taji la Red...

MCAs kutumia Sh10 milioni katika warsha Mombasa

T L