Michezo

Yaliyopita si ndwele: Arsenal yaandaa risasi za kuvizia Wolves kutafuta alama tatu EPL

April 20th, 2024 1 min read

LONDON, UINGEREZA

RISASI za Arsenal zipo ama zimeisha? Swali hilo litapata jibu leo wakati wanabunduki hao watarejelea majukumu ya Ligi Kuu dhidi ya wenyeji Wolves ugani Molineux.

Ni mechi yenye umuhimu mkubwa kwa nambari mbili Arsenal ambao wana fursa ya kuruka juu ya jedwali ikiwa watapita mtihani mkali kutoka kwa mbwa mwitu hao wanaokamata nafasi ya 11.

Vijana wa kocha Mikel Arteta wana alama 71, mbili nyuma ya viongozi Manchester City ambao wanavaana na Chelsea katika nusu-fainali ya Kombe la FA ugani Wembley Jumamosi.

Arsenal wamezoa ushindi mara tano mfululizo dhidi ya Wolves kwa jumla ya mabao 12-2.

Walipepeta wenyeji wao 2-0 kupitia mabao ya nahodha Martin Odegaard mara ya mwisho walipozuru Molineux mnamo Novemba 12, 2022.

Odegaard ni mmoja wa wachezaji watakaotegemewa na Arsenal katika mchuano huo wao wa 33 wa ligi bila ushindi katika mechi tatu kwenye mashindano yote.

Arsenal, ambao hawajashinda ligi kwa miaka 20, walipoteza fursa ya kutwaa uongozi baada ya kuchapwa 2-0 na Aston Villa ugani Emirates wikendi iliyopita.

Wolves nao hawana ushindi mara tano katika mashindano yote msimu huu na wamepoteza mara mbili mfululizo mikononi mwa Arsenal ugani Molineux.

Kocha Gary O’Neil ana wachezaji kadhaa wakutegemea akiwemo Matheus Cunha.

Jumamosi pia ni zamu ya Luton Town kutafuta ushindi wa kwanza dhidi ya Brentford baada ya kupoteza tatu mfululizo. Walicharazwa 5-1 na City mnamo Aprili 1.

Nao Brentford wamejaa motisha kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Sheffield United.

Sheffield watakuwa wenyeji wa Burnley. Luton, Burnley na Sheffield zinakamata nafasi tatu za mwisho za kuangukiwa na shoka kwa hivyo kila mmoja atajituma vilivyo kufufua matumaini ya kusalia ligini.

Aidha, Man-City ya kocha Pep Guardiola haijapoteza dhidi ya Chelsea ya kocha Mauricio Pochettino mara nane mfululizo, hivyo ina motisha ya kufana leo pia.

Nusu-fainali nyingine itakutanisha Coventry City na Manchester United Jumapili.