Michezo

Yanga wakataa kuabiri basi la Gor wakidai lina uchawi

July 18th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Yanga SC walikataa kuliabiri basi walilokuwa wamekodishiwa na Gor Mahia katika uwanja wa ndege wa JKIA wakidai kwamba lilikuwa limetiwa nguvu za giza, uchawi.

Wageni hao badala yake waliamua kutumia usafiri wa umma kwa kuabiri basi la City Hoppa katika kisa kilichozua ‘drama’ kubwa uwanjani humo.

Kando na hayo majagina hao wa soka ya Tanzania pia walikataa kutumia hoteli waliyokodishiwa na badala yake wakafululiza hadi hoteli waliyojikodishia wenyewe inayopatikana kwenye barabara ya Thika.

“Walikataa kuabiri basi walilotengewa kisha wakajitoma ndani ya City Hoppa na kuelekea kwa hoteli waliyojikodishia.  Walitoa  sababu za uchawi na shauku ya kutiliwa mazingaombwe kwenye vyumba walivyokodishiwa,” ikasema taarifa kutoka kwa Gor Mahia.

Timu hizo mbili zinatarajiwa kuchuana kwenye kipute cha kombe la mashirikisho CAF Jumatano 18 2018, huku kila timu ikilenga kusajili ushindi wake wa kwanza.

Gor wameandikisha alama mbili baada ya kusajili sare dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda na USM Alger kutoka Algeria.

Yanga SC kwa upande wao walipoteza mechi zao mbili za kwanza na ushindi utafufua jitihada zao na kuwaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu raundi ya mwoondoano

Swala la ‘dumba’ si geni kwa klabu hizo mbili. Mwaka wa 2016 Yanga SC walikataa kuabiri basi walilokodishiwa na Rayon Sports wakati wa mechi ya kombe la mashirikisho, CAF nchini Rwanda. Mwaka huo walidai kwamba basi hilo lilikuwa limetiwa urogi.

Gor Mahia nao juzi walikataa kutumia chumba cha kubadilisha nguo kabla ya mechi yao ya nusu fainali dhidi ya Azam kwenye mashindano yaliyokamilika ya CECAFA Kagame Cup wakihofia madhara ya dumba

Hata hivyo waliishia kupoteza mechi hiyo kisha wakagomea kupokea medali ya fedha baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu.