Habari Mseto

Yashukiwa mwanafunzi alikufa kwa kupigwa shuleni

June 10th, 2019 2 min read

NA NICHOLAS KOMU

UTATA unaozingira kifo cha mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya upili ya Wasichana ya Bishop Gatimu Ngandu aliyedaiwa kujitia kitanzi umechukua mwelekeo mwingine, madai yakizuka kwamba huenda binti huyo alipigwa siku moja kabla ya mauti yake.

Ingawa matokeo ya uchunguzi wa maiti yalionyesha alijinyonga, maelezo mapya yanaashiria kwamba marehemu Joan Mumbi alikuwa na majeraha ya kichwa kabla ya kupatikana ameaga dunia.

Wazazi wake na baadhi ya wanafunzi wenzake wamekanusha kwamba mwendazake aliyezikwa majuma mawili yaliyopita eneo la Tetu, alijitoa uhai na kutaka uongozi wa shule kutoa maelezo kuhusu kilichosababisha mauti yake.

“Msichana wangu hakujiua. Najua wengi wanasema hivyo ila siwaamini kabisa. Kuna jambo lililotokea usiku huo na tunahitaji majibu,” akasema babake Georege Kariru wakati wa mahojiano na Taifa Leo nyumbani kwake Magayu-ini, Tetu.

Ripoti za polisi zilionyesha mwili wa Bi Mumbi ulipatikana umening’inia kwenye paa la bweni mnamo Mei 19, hali iliyoonyesha wazi kwamba alijitia kitanzi.

Vile vile maelezo mengi yaliyopatikana kwenye karatasi ndani ya dawati lake, yalionyesha alikuwa akikumbwa na msongo wa mawazo kutokana na shinikizo za kumtaka afanye vizuri masomoni.

Polisi sasa wanaendeleza uchunguzi zaidi kuhusu kifo hicho baada ya wazazi kushikilia kwamba mwanao hakujinyongana na pia hakuwa akikumbwa na msongo wa mawazo

“Joan si mtu yule anayenyamazia shida zake. Alikuwa akitueleza masaibu yake kila mara alipokumbana nayo. Madai kuhusu msongo wa mawazo yalitungwa ili kufunika ukweli,” akasema Mamake Edda Wanjiku.

Taifa Leo pia ilipata maandishi kutoka kwa mwanafunzi ambayo yanaonyesha jinsi walivyoshuhudia Bi Mumbi akiadhibiwa vikali na walimu na pia wakashikilia hakujinyonga.

“Hatujui kile uongozi wa shule umekueleza lakini ukweli ni kwamba Joan alianguka mtihani wa majaribio kwenye Kemia na akaingiwa na wasiwasi wa kutoafikia malengo ya mamake. Alijaribu kubadilisha matokeo lakini akapatikana,” ikaanza barua hiyo.

“Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo, alisema hakufurahia kufeli. Alichapwa vibaya na walimu na wakamwambia abebe sanduku lake aende kwa afisi ya Naibu Mwalimu Mkuu,” ikasema barua hiyo.