Yatani kutuma Sh39 bilioni kwa kaunti baada ya magavana kutisha kusitisha huduma

Yatani kutuma Sh39 bilioni kwa kaunti baada ya magavana kutisha kusitisha huduma

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha Ukur Yatani Jumanne alisema Hazina ya Kitaifa itatuma Sh39 bilioni kwa serikali za kaunti mwishoni mwa wiki hii.

Waziri ametoa tangazo hilo siku moja baada ya magavana kutisha kuzimisha shughuli katika kaunti zote 47 endapo kufikia Ijumaa Hazina ya Kitaifa haitakuwa imetoa jumla ya Sh102 bilioni ambazo serikali hizo zinadai.

Pesa hizo ni sehemu ya mgao wa Sh316.5 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 unafikia kikomo Juni 30, 2021.

Hata hivyo, Bw Yatani ambaye Jumanne alifika mbele ya Kamati ya Seneta kuhusu Bajeti na Masuala ya Fedha alisema kuwa baadhi ya serikali za kaunti huwa hazitumii fedha zilizotengewa na zile kutoka wafadhili.

“Licha baadhi ya kaunti zinalalamikia kucheleweshwa kwa mgao wao wa fedha, kuna magavana ambao pesa zao zingali katika akaunti za kaunti zao katika Benki ya Kuu,” akawaambia wanachama cha kamati hiyo wakiongozwa na Seneta wa Kirinyaga, Charles Kabiru.

“Tutatoa pesa jumla ya Sh39 bilioni Ijumaa au Jumatatu. Pesa hizi ni mgao wa mwezi Machin a Aprili. Vile vile, nawaomba mzihimize kaunti ambazo hazijatumie pesa zao zisiache katika akaunti zao za Benki ya Kitaifa,” Bw Yatani akasisitiza.

Mnamo Jumatatu, mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora alilalamika kucheleweshwa kwa fedha ambazo kaunti zinadai Hazina ya Kitaifa kumechangia serikali hizo kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati na wafanyabiashara wanaoziwasilishia bidhaa kwa mkopo.

Vile vile, wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali inayofadhiliwa na kaunti wameathirika kutokana na kucheleweshwa kwa fedha hizo.

“Kaunti iliyoathirika zaidi ni Nairobi ambayo haijalipwa fedha za hadi miezi sita,” Bw Wambora akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu.

“Ikiwa Hazina ya Kitaifa haitatoa jumla ya Sh102 bilioni ambazo tunazidai kufikia Ijumaa, hatutaweza kutoa huduma za kimsingi pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi. Hali ikiendelea hivyo, tutalazimika kusitisha kabisa huduma ifikapo Juni 24, “ mwenyekiti huyo ambaye ni Gavana wa Embu akasema kwenye taarifa hiyo.

You can share this post!

Wavuvi Lamu wadai maegesho yao yamenyakuliwa

Ronaldo avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye soka ya...