Yattani apondwa kuhusu ongezeko la deni la kitaifa

Yattani apondwa kuhusu ongezeko la deni la kitaifa

Na David Mwere

IDARA ya Bunge kuhusu Bajeti (PBO) sasa inalaumu Wizara ya Fedha kwa deni kubwa la kitaifa ambalo linaendelea kuongezeka.Idara hiyo ambayo hutoa ushauri kuhusu masuala ya bajeti za taifa inasema kwamba deni hilo linaongezeka kwa sababu ya ukosefu wa mikakati mizuri katika wizara hiyo.

Licha ya lawama hizo, ofisi hiyo inasema kwamba Kenya haina budi kuendelea kukopa ili kufadhili bajeti ya mwaka wa 2021/22 kufuatia kupungua kwa mapato janga la corona lilipovuruga uchumi.

Hata hivyo, ili kuendelea kukopa, wizara ya fedha italazimika kushawishi bunge kubadilisha sheria ya usimamizi wa fedha za umma ya 2015 kuongeza kiwango cha deni la kitaifa. Kwa sasa, Kenya haiwezi kukopa zaidi ya Sh9 trilioni.

“Kuna madai ya ukosefu wa uadilifu kuhusu usimamizi wa fedha katika wizara ya fedha,” ripoti ya hivi punde ya PBO inasema.Waziri wa Fedha Ukur Yattani hakujibu maswali yetu kuhusu madai ya PBO, ambayo inashauri bunge kuhusu masuala ya bajeti.

Madai ya PBO yanajiri huku wizara ya Fedha ikiwasilisha pendekezo la kuongeza kiwango cha deni la kitaifa kwa Sh 3 trilioni hadi Sh12 trilioni.

Mnamo Novemba , 2019, bunge iliongeza kiwango cha deni la serikali hadi Sh9 trilioni na kufikia Septemba 2020, deni hilo lilikuwa Sh8.41 trilloni kumaanisha nchi imebakisha Sh590.92 billoni kutimiza kiwango kilichowekwa.

PBO inahofia kwamba kukiwa na upungufu wa Sh1.059 trilioni katika bajeti ya mwaka huu, kiwango cha deni kitafikiwa kufikia Juni mwaka huu.

“Ikizingatiwa upungufu katika bajeti kwa wakati huu, kiwango cha deni kinaweza kufikiwa kufikia mwisho wa Juni 2020/21,” PBO inaonya ikisema Kenya haiwezi kuepuka kukopa kufadhili bajeti yake.Sehemu ya 50 (2) ya sheria ya usimamizi wa fedha inaruhusu serikali ya kitaifa kukopa bila kupitisha kiwango kilichowekwa na bunge.

You can share this post!

DINI: Matunda ya kesho yako kwenye mbegu za leo kwa hivyo...

Chama cha Pwani ni Kadu Asili – Jumwa