Michezo

YATUA: Harambee Stars yatua Misri tayari kwa kibarua kigumu

June 20th, 2019 2 min read

Na HRIS ADUNGO na MASHIRIKA

ZILIKUWA mbwembwe, vifijo, hoihoi na nderemo kikosi cha Kenya kilipotua Jumatano usiku jijini Cairo, Misri kwa ajili ya kabumbu maarufu zaidi barani, Kombe la Afrika, linalong’oa nanga Ijumaa.

Kikosi cha Harambee Stars kilichovalia makoti meusi na long’i aina ya khaki kililakiwa kwa furaha na nyimbo za kizalendo zilizoimbwa na Wakenya wanaoishi nchini humo punde kilipowasili katika makazi yake kwa basi jeusi lililochorwa bendera ya Kenya.

Harambee Stars inayorejea katika mashindano hayo baada ya kukaa nje kwa miaka 15, imetiwa katika kundi gumu linalojumuisha Algeria, Senegal na Tanzania.

Huku waliowalaki wakihakikisha kuwa wamesalimu kila mchezaji kwa mikono, macho yote yalielekezwa kwa wanasoka mahiri wanaosakata kabumbu katika mataifa ya ughaibuni.

Kiungo matata wa Tottenham Hotspur, Victor Wanyama alishangiliwa pakubwa.

Hata hivyo, masogora wengine kama vile Michael Olunga anayesakatia Kashiwa Reysol ya Japan na Ayub Timbe anayechezea Beijing Renhe ya Uchina hawakusahauliwa katika mapokezi hayo ya aina yake.

Ayub Timbe (kushoto) wa Kenya apambana na mwanasoka wa Madagascar katika mechi ya kirafiki jijini Paris mnamo Ijumaa (7/6/2019). Picha/ Hisani

Kikosi cha Harambee Stars kina siku tatu zaidi za kuzoea joto jingi la Misri kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Algeria katika mechi ya ufunguzi wa Kundi C katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) hapo Jumapili.

Chini ya mkufunzi Sebastien Migne, Stars walitua jijini Cairo mnamo Jumanne usiku baada ya kuondoka Paris, Ufaransa walikokuwa wakipiga kambi kwa siku 19.

Baada ya kuchuana na Algeria wanaojivunia huduma za kiungo matata wa Manchester City Riyad Mahrez, Stars watashuka dimbani kupimana ubabe na majirani zao Tanzania hapo Juni 27 kabla ya kufunga kampeni za makundi dhidi ya wanafainali wa 2002, Senegal siku ya Julai 1.

Wakiwa Ulaya, Stars walipiga michuano miwili ya kujipima nguvu. Waliwachabanga Madagascar 1-0 jijini Paris, Ufaransa kabla ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi ya pili iliyochezewa jijini Madrid, Uhispania.

Michuano hiyo ilimpa Migne jukwaa maridhawa la kupima uwezo wa kila mchezaji katika orodha ya masogora 23 anaojivunia kwa sasa kikosini.

Ingawa hivyo, Stars watazikosa huduma za nahodha msaidizi, Musa Mohammed ambaye alipata jeraha la goti wakicheza dhidi ya Madagascar.

Beki huyo wa klabu ya Nkana Red Devils nchini Zambia anatarajiwa kusalia nje ya kikosi cha Stars katika mchuano wa ufunguzi dhidi ya Algeria.

Ni wakati wakiwa Paris ambapo Stars walikabiliwa pia na pigo la kuzikosa huduma za beki Brian Mandela wa Maritzburg United kutoka Afrika Kusini. Mandela alipata jeraha la goti ambalo lilimweka nje ya kampeni zote za makala ya 32 ya AFCON.

Kukosekana kwa wawili hao kunamweka Migne katika ulazima wa kuwategemea Joash Onyango, Joseph Okumu, David ‘Calabar’ Owino na Bernard Ochieng katika safu ya ulinzi ya Stars.

Baada ya kuridhisha zaidi wakicheza dhidi ya DR Congo, Onyango na Okumu wanatarajiwa kuunga kikosi cha kwanza cha Stars kitakachowajibika dhidi ya Algeria.

Licha ya jeraha, Mandela aliyeonekana akitembea kwa usaidizi wa mikongojo, alikuwa sehemu ya wachezaji walioandama na wenzake wa Stars nchini Misri mnamo Jumanne.

Stars wanahitaji ushindi dhidi ya Algeria ili kupata hamasa tele zaidi ya kutatiza Tanzania na kuwatikisa Senegal wanaojivunia huduma za mvamizi Sadio Mane wa Liverpool, Uingereza.

Algeria watashuka dimbani wakitawaliwa na ghera ya kuendeleza ubabe ambao umewawezesha kung’aa katika maandalizi baada ya kusajili ushindi mara sita, kupiga sare tatu na kupoteza mchuano mmoja kati ya 10 iliyopita. Kwa upande wao, Stars wameshinda mechi sita, kusajili sare mbili na kupoteza moja kati ya 10 zilizopita.