Dondoo

Yaya ajuta kugeuza nyumba ya mdosi kuwa danguro

April 22nd, 2018 1 min read

Na SAMMY WAWERU

FREE AREA, NAKURU

Yaya aliyekuwa akifanya kazi kwa mama mmoja mtaani hapa, anajuta baada ya kupigwa kalamu kwa kuhangaisha wanaume.

Duru zinasema mwanadada huyo aliajiriwa Desemba 2017 ili kumsaidia bosi wake aliyejifungua.

Mama huyo alirejea kazini mwezi uliopita, na kipusa amekuwa akialika wanaume tofauti kwa mwajiri wake.

Kulingana na mdaku wetu  hata kazi aliyoajiriwa kufanya ilimshinda sababu alikuwa bize akipokea wageni.

“Kidosho mwenyewe ni mrembo ma huvalia mavazi  ya hadhi ya juu,” alisema mdokezi.

Majirani walimfahamisha dosi tabia za yaya wake, lakini alimtetea akisema hakuona makosa yoyote kwake.

“Huyu ni msichana mdogo hajui mambo ya wanaume,” mama alimjibu jirani mmoja.

Inasemekana hivi majuzi kipusa alialika jamaa mmoja baada ya kukamilisha majukumu aliyopewa.

Wakiwa katika harakati za mahaba sebuleni mapolo wawili walifika, wote wakidai yaya huyo alikuwa mpenzi wao. Walianza kubishana na mwishowe wakalishana makonde.

“Hayo mavazi anayovalia mnajua bei yake kweli? Mimi ndiye humnunulia,” aliwaka kalameni mmoja, wote wakikabana koo.

Kuna aliyedai kuwa kipusa alitoka kwao na kwamba alikuwa mchumba wake.

“Huyu mimi ndiye nilimleta huku kwa kuwa tumetoka mahali moja, na ni mke wangu,” alilalamika.

Polo wa tatu alisema bosi wa yaya ni rafiki wa dhati na alijua uhusiano wao.

Yasemekana majirani ndio waliingilia kati na kufurusha makalameni hao wakitishia kuwacharaza endapo wangeendelea kuzua fujo tena.

Mama alifika makalameni walipokuwa wakizozana na kujionea sinema hiyo. Kipusa alisalia kimya akishindwa kujitetea kwa mshtuko aliopata.

Inasemekana dosi alimlipa mshahara wake na kumfurusha kisha akawaomba radhi majirani zake na kuwashukuru kwa kumfunua macho.

…WAZO BONZO…