Habari Mseto

Yaya anaswa na kamera akimtwanga mtoto wa miezi mitatu

May 27th, 2019 1 min read

Na Evelyne Musambi

MWANAMKE wa miaka 31 ambaye ni mfanyakazi wa nyumbani alipatikana akimchapa mtoto wa miezi mitatu wakati alipokuwa akimnywesha maziwa kwa chupa, baada ya kamera kumrekodi akifanya hivyo.

Mfanyakazi huyo kwa jina Irene Nzisa alikuwa ameajiriwa mwezi mmoja na nusu uliopita katika nyumba moja mtaa wa Mlolongo, kuwa akiwalea watoto wawili.

Mwajiri wake aliweka kamera sebuleni ili kumsaidia awe akifuatilia yanayoendelea wakati hayuko.

Mnamo Jumatatu, mwajiri huyo alishtuka wakati aliondoka nyumbani kumpeleka bintiye mkubwa hospitalini, lakini alipokuwa akifuatilia kamera ya nyumbani akamwona Nzisa akimchapa malaika huyo.

Kanda ya kuonyesha matukio hayo ilionyesha Nzisa akimpa mtoto huyo maziwa, kisha wakati fulani akawekelea chupa ya maziwa mezani na kuanza kumpiga mtoto huyo mikononi na mapajani.

Baada ya muda, aliacha kumpa maziwa na kumweka katika kiti chake, akimyooshea kidole kwa hasira.

“Nilishtuka, hatukufika hospitalini baada ya kuona hivyo. Nilirudi nyumbani mara moja na nikampigia mume wangu aje na polisi,” akasema mama huyo.

Nzisa alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha Mlolongo, kabla ya kuachiliwa siku iliyofuata.