Habari Mseto

Yaya kizimbani kwa kuiba chupi za bosi wake

February 8th, 2019 1 min read

Na Titus Ominde

KIJAKAZI mmoja Alhamisi alishtakiwa katika mahakama moja mjini Eldoret kwa kumwibia mwajiri wake chupi na nguo nyingine.

Yaya huyo ambaye aliambia mahakama ana umri wa miaka 16 alikabiliwa na mashtaka kumwibia mwajiri wake chupi nne, sodo tano, sidiria, miswaki, long’i sita, vipodozi, shati sita, begi miongoni mwa vifaa vingine vya nyumbani vya kima cha Sh110,000.

Mahakama iliambiwa kuwa mshtakiwa alitekeleza wizi huo mnamo Februari 2, 2019 katika mtaa wa Kapsoya mjini Eldoret.

Binti huyo ambaye alionekana kushtushwa na hatua ya mwajiri wake kumfikisha kortini alikana mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Eldoret Bw Harrison Barasa.

Hakimu aliamuru mshtakiwa kupelekwa katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi MTRH kufanyiwa uchunguzi wa umri.

Vilevile, mahakama iliamuru mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 la sivyo azuiliwe katika rumande ya watoto mjini Eldoret.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Februari 12.