Dondoo

Yaya mlishwa makombo atafuna mayai ya mdosi

April 3rd, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KIAMBERE MJINI

KIJAKAZI mmoja kutoka mjini hapa alizua kioja plotini alipotafuna mayai ya mdosi wake na kutishia kumshtaki kwa wazazi wake kwa kumbagua.

Penyenye zinasema mdosi aliahidi wazazi wa kijakazi huyu kuwa angemtunza vyema binti yao lakini baada ya mwezi mmoja demu alianza kulalamika  kwamba hakuwa akila chakula bora kama mdosi na familia yake.

Wakati mwingine msichana huyu alilazimika kula mabaki ya chakula chao. Siku ya tukio kijakazi aliamka asubuhi na mapema kupikia mdosi chai na mayai lakini baada ya kutayarisha staftahi hiyo,  alitafuna mayai.

Mdosi alipoamka alishangaa sana kupata kijakazi akiwa tayari ametafuna mayai yake na kujilaza kochoni huku akitazama runinga na hapo ndipo akaanza kumfokea.

“Yaani ulipika mayai yangu na ukayala bila ruhusa yangu. Nataka mayai yangu sasa hivi,” mdosi alijaribu kurukia kijakazi kwa hamaki amlishe kichapo lakini msichana alimzidi maarifa.

“Usijaribu kunigusa. Umenitesa kwa muda mrefu ukidhani mimi ni zuzu. Leo ni mimi nitakula chakula bora kuliko nyinyi. Tangu uniajiri umekuwa ukinibagua.

Unakula chakula kizuri pamoja na familia yako huku mimi nikila mabaki ya chakula chenu.

Nitawaambia wazazi wangu kila kitu. Uliawaahidi kuwa mtanitunza lakini wewe ni bure kabisa. Umenitenga na kuniona kama takataka mbele yenu,” kijakazi alifoka.

Hali ilizidi kuchacha hadi wapangaji wakakusanyika kujionea sinema hiyo ya bure. Cha kushangaza ni kuwa wakati mdosi alipoona angeaibishwa kabisa, alifurusha waliokuja kuwatazama.

Hata hivyo, alikemewa na watu na ikamlazimu aondoke kuenda zake akihofia ghadhabu ya watu hao.

Kutoka siku hiyo, hakumtesa msichana huyo tena ambaye tunafahamishwa kwamba alikuwa mchapakazi na mkali kwa kutetea haki zake.

…WAZO BONZO…