Dondoo

Yaya pabaya kuandalia bosi minofu

October 8th, 2019 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

BROOKE, KERICHO

MWANADADA wa hapa alimchemkia yaya wake kwa kumwandalia mumewe mapochopocho badala ya ugali kwa sukumawiki alivyokuwa amemwamuru.

Mdaku wa makala haya anaarifu kuwa ndoa kati ya mwanadada na mumewe inayumbayumba baada ya kukabiliwa na misukosuko kadhaa.

“Mambo yalikuwa shwari hadi alipomfumania jamaa akiwasiliana na kisura kupitia mtandao wa kijamii. Kidosho aliwaka kwani wawili hawa walikuwa wakibadilishana jumbe zilizojaa maneno ya mahaba,” mdaku aliarifu.

Hata hivyo, jamaa alifaulu kumlilia mwanadada amsamehe na kumpa nafasi ya mwisho katika ndoa.

Mwanadada alimsamehe lakini hakusahau kamwe kusalitiwa na mumewe.

Mambo yalizidi unga kwa polo alipopoteza kazi yake kwani kandarasi yake kwenye kampuni moja ilifika mwisho na hakupewa nafasi tena.

“Mkewe alianza kumdharau kwani jamaa alimtegemea kwa kila kitu. Kipusa huyo alinukuliwa akisema kuwa mumewe hakustahili heshima kwa maana alifuja hela zake akiponda raha na visura,” mdaku alieleza.

Juzi, alikuwa na safari na akamwagiza yaya wake kuwa ikitimia saa sita ya mchana apike sembe kwa sukumawiki kisha amwandalie mumewe akisema angerudi usiku.

Hata hivyo, alirudi mapema mno na kupandwa na mori kupata demu akiwa ameandalia jamaa na rafiki yake aliyekuwa amemtembelea mlo sphesheli.

Kilichoudhi mwanadada hata zaidi ni kwa yaya kusema kwamba alikopa nyama.

“Mgeni alipoingia nilichomoka kukopa nyama kilo moja kwa ahadi kuwa ungelipa ukirudi,” yaya aliungama na mama akachemka hata zaidi.

“Nani alikuambia unitie kwenye gharama kulisha malofa wanaokaa tu kupiga gumzo? Nitakata mshahara wako mwezi huu kufidia hasara hii,” mke wa mtu alimfokea kidosho mumewe na mgeni wakiduwaa tu.