Habari Mseto

Yaya wa Wanjigi ana kesi ya kujibu – Mahakama

June 13th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

YAYA wa aliyekuwa waziri Maina Wanjigi (pichani) ametakiwa kujitetea kesi aliyoshtakiwa pamoja na mwanamke mwingine kwa kumnyang’anya mwajiri wake bunduki mbili, risasi, pesa na simu miaka mitano iliyopita.

Hakimu Mkuu wa Kibera Joyce Gandani alimwambia Dorcas Mumbi Kitili kwamba ushahidi uliotolewa kortini unaonyesha ana kesi ya kujibu na anafaa kujitetea.

Bi Mumbi anayewakilishwa na wakili John Swaka ameshtakiwa pamoja na Bi Hilda Nabweko kwa kutumia nguvu kumnyang’anya mzee Wanjigi bastola aina ya Ceska iliyokuwa na risasi 14, bunduki aina ya Weston iliyokuwa na risasi sita, saa ya mkono aina ya Rolex, Sh17,000 pesa taslimu na simu mbili za mkono miongoni mwa bidhaa nyingine.

Kulingana na mashtaka na ushahidi uliotolewa kortini, wakati wa kisa hicho, wawili hao na washukiwa wengine ambao hawakukamatwa walitumia bastola, simi na visu kumtisha Bw Wanjigi na watu wa familia yake.

Kwa jumla wanakabiliwa na mashtaka matatu ya wizi wa mabavu wanayodaiwa kutekeleza dhidi ya watu waliopata katika nyumba ya Bw Wanjigi.Mahakama ilifahamishwa kwamba walimtisha na kumnyang’anya Bi Florence Gitungo simu ya mkono aina ya Nokia ya thamani ya Sh7000.

Kwenye shtaka la tatu ilidaiwa kwamba walitumia nguvu kumnyang’anya Bi Eunice Nungari simu yake.Bi Nabweko anakabiliwa na shtaka la ziada la kupatikana na simu ambayo Bi Nungari alinyang’anywa wakati wa kisa hicho.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba alipatikana na simu hiyo Novemba 29 2013 katika mtaa wa Kibera, siku saba baada ya Bw Wanjigi kuvamiwa na wezi nyumbani kwake na kuibiwa mali.Bi Mumbi aliambia mahakama kwamba anahitaji rekodi zote za kesi ili ajiandae kujitetea, ombi ambalo lilikubaliwa.

Bi Gandani aliagiza wafike kortini Agosti 21 kujitetea.