Michezo

Yego afuzu fainali za kurusha mkuki Olimpiki

Na BERNARD ROTICH August 6th, 2024 1 min read

ALIYEKUWA bingwa wa kurusha mkuki, Julius Yego amefuzu fainali ya kuwania ubingwa wa Michezo ya Olimpiki.

Yego alifuzu baada ya kurusha kwa umbali wa mita 85.97m, umbali ambao ni bora zaidi kwake msimu huu. Alimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Julian Weber aliyerusha kwa umbali 85.76m, huku Yakub Valdlejch wa Croatia aliyemaliza katika nafasi ya tatu akirusha kwa umbali wa 85.63m.

Katika jaribio la kwanza, Yego alirusha umbali wa 78.84m, kabla ya kupanda hadi 80.76m na baadaye 85.97m kwenye jaribio la mwisho.

Yego hakufika fainalini michezo hiyo ilipofanyika Tokyo mnamo 2020 alikomaliza katika nafasi ya 24 baada ya kurusha kwa umbali wa 77.34m. Baadaye alirusha kwa umbali wa 79.62 na kutwaa ubingwa wa Afrika Michezo ya Bara ilipofanyika Port Louis nchini Mauritius.

Katika mashindano ya Dunia yaliyofanyika Oregon nchini Amerika, Yego alimaliza katika nafasi ya 14 baada ya kurusha kwa umbali wa 78.42m. yalipofanyika mwaka uliopita mjini Budapest, alikuwa na kiwango cha chini aliporusha kwa 78.42m.

Mwaka huu alianza kwa nishani ya Fedha mjini Accra, Ghana mwezi Machi alikorusha kwa 81.74m, kabla ya kutwaa ushindi wa Afrika mjini Douala, Cameroon mwezi Juni kwa kurusha kwa 80.24m.