Yego nje ya Olimpiki

Yego nje ya Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa dunia wa kurusha mkuki mwaka 2015, Julius Yego amebanduliwa kwenye Olimpiki 2020 katika raundi ya kwanza jijini Tokyo, Japan mnamo Jumatano.

Yego, 32, ambaye anashikilia rekodi ya Kenya na Afrika ya mtupo wa mita 92.72 kutoka mashindano ya dunia ya 2015 jijini Beijing nchini Uchina, alikamilisha kampeni yake ya Tokyo kwa kurusha mkuki huo wa urefu sentimita 259.04 na gramu 798.3 umbali wa mita 77.34 katika kundi la pili.

Bingwa huyo wa Afrika 2012, 2014 na 2018 na Jumuiya ya Madola 2014, ambaye alishinda nishani ya fedha kwenye Olimpiki 2016 nchini Brazil, hakufanikiwa katika mitupo yake miwili ya kwanza kabla ya kuandikisha matokeo hayo yake bora msimu huu katika jaribio la tatu.

Arshad Nadeem (Pakistan), Jakub Vadlejch (Czech) na Julian Weber (Ujerumani) walifuzu kushiriki fainali kutoka kundi hili baada ya kukamilisha mchujo huo wa watu 16 kwa kurusha mkuki umbali wa mita 85.16, mita 84.93 na mita 84.41, mtawalia.

Neeraj Chopra (India) alishinda kundi la kwanza kwa mita 86.65 akifuzu moja kwa moja kwa kumaliza katika nafasi tatu za kwanza pamoja na Mjerumani Johannes Vetter (85.64) na raia wa Finland Lassi Etelatalo (84.50).

Fainali ya kurusha mkuki ni Agosti 7. Itahusisha warushaji 12 waliokuwa na mitupo kati mita 82.40 na 86.65 jijini Tokyo.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yatoa Sh17.4 bilioni kufadhili masomo katika shule...

Barshim na Tamberi wagawa dhahabu ya Olimpiki katika fani...