Michezo

Yerry Mina kukosa mechi ya Liverpool

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata wa Everton, Yerry Mina atakosa mchuano wa kwanza wa kurejelewa kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupata jeraha la mguu akishiriki mazoezi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Everton, sogora huyo mzawa wa Colombia alipata jeraha la misuli kwenye mguu wake wa kushoto.

Atasalia mkekani kwa “majuma kadhaa” na huenda akakosa kunogesha gozi la Merseyside litakalowakutanisha Everton na Liverpool baada ya soka ya muhula huu kuanza upya.

Mina, 25, kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa matabibu wa kikosi cha Everton uwanjani Goodison Park. Hadi kufikia sasa, Yeri anajivunia kuwajibikia Everton katika jumla ya mechi 25.