Kimataifa

'Yesu' na wafuasi wake wakamatwa wakisubiri dunia iishe

September 27th, 2018 1 min read

DAILY MONITOR NA PETER MBURU

Kampala, Uganda

MWANAMUME anayejiita Yesu Kristo alikamatwa pamoja na wafuasi wake katika Wilaya ya Lira, Uganda Jumanne jioni baada ya kuuza mali yao wakidai kuwa nyakati za mwisho zimewadia.

Polisi nchini humo walisema walimkamata Alex Okello kutoka alikokuwa mafichoni Kaunti-Ndogo ya Barr, muda baada ya wafuasi wake 14 kukamatwa Oktoba.

Polisi waliwakamata 14 hao wakati walivamia kambi yao na kuwapata wakisubiri mwisho wa dunia, baada ya kuuza mali yao, japo wakati huo Bw Okello alikuwa ameenda mafichoni.

“Sasa tumemkamata na tuko naye pamoja na wafuasi wake humu ndani,” afisa wa polisi anayefuatilia kesi hiyo  katika kituo cha polisi cha Lira Central alieleza shirika la habari la Daily Monitor Jumatano.

Alisema hadi waliposhikwa washukiwa Jumanne bado hawakuwa wamekubali kuzungumza.

“Tutakapoanza kuchukua habari zao ndipo tutabaini nini ilikuwa nia yao na ndipo tutabaini mashtaka ambayo tutawafungulia,” akasema.

Msemaji wa polisi eneo la Kyoga Kaskazini David Ongom Mudong alithibitisha kukamatwa kwa 15 hao akisema, “walipofikishwa katika kituo cha polisi cha Lira Central Jumanne, washukiwa hawakuwa wakizungumza. Lakini leo (Jumatano) tunataka kuwahoji ili kubaini lengo lao.”

Wafuasi waliojiita wanafunzi wa mwanamume huyo waliuza mali yao na ya familia zao baada ya kuamrishwa naye na walikuwa wamepiga kambi kijiji cha Akwo, eneo la Abunga ambapo walikuwa wakisubiri dunia kuisha Oktoba 2018.