Michezo

Yidah avunja ndoa na Sharks na kuyoyomea Nairobi City Stars

September 11th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mvamizi wa Harambee Stars U-23, Sven Yidah, amejiunga na Nairobi Stars kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuagana na Kariobangi Sharks aliowachezea kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Yidah, ambaye pia alikuwa akihusishwa pakubwa na AFC Leopards na Yanga SC ya Tanzania, alisajiliwa na Sharks mnamo 2016 baada ya kukatiza rasmi uhusiano wake na klabu ya Ligi Ndogo.

Sogora huyo anakuwa wa sajili wa sita kuingia kambini mwa City Stars ambao wamepania kurejea kwenye kivumbi cha Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa matao ya juu baada ya kutawala Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) mnamo 2019-20.

“Najiunga na City Stars baada ya kupokezwa malezi bora ya soka katika kikosi cha Sharks. Kilichonichochea kuagana na Sharks ni kukosekana kwa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza katika kampeni za msimu uliopita. Naamini City Stars watanipa jukwaa mwafaka zaidi la kukua kitaaluma na kuimarika zaidi kisoka,” akasema Yidah.

“Nimeridhishwa na mseto mzuri wa wachezaji wazoefu na chipukizi kambini mwa City Stars ambao tayari wametufichulia malengo yao ya muhula ujao,” akaongeza.

Yidah anaungana na wachezaji Yusuf Lubowa Mukisa, Erick Ombija, kipa Elvis Ochieng Ochoro (Hakati Sportiff), Ronney Kola Oyaro (Kenya School of Government (KSG)), Rowland Makati (Vapor Sports) na Timothy Ouma (Laiser Hill Academy) ambao wamesajiliwa na City Stars katika kipindi cha majuma machache yaliyopita.

Akiwa kambini mwa City Stars, Yidah ataendelea kuvalia jezi nambari 18 aliyokuwa akivalia katika kikosi cha Sharks aliowachezea jumla ya mechi 97 tangu 2017.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 alikuwa sehemu muhimu katika kampeni za Sharks waliotawazwa mabingwa wa SportPesa Cup mnamo 2019 jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Kwa kutua City Stars, Yidah anaungana na wanasoka Ebrima Sanneh, Shittu Salim Abdalla na Wycliffe Otieno waliowahi kucheza pamoja naye katika kikosi cha Sharks.