Michezo

Young Achievers yaibuka mabingwa

August 23rd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Young Achievers ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 12 imetawazwa mabingwa wa taji la KYSD kwenye mechi zilizoandaliwa katika Uwanja wa KYSD, Majengo Nairobi.

Y Achievers ya kocha Hamza Kipkemoi kutoka Kitui Village ilitwaa ubingwa huo baada ya kunyamazisha wapinzani wao Green Rhino FC kwa mabao 2-1 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika muda wa kawaida.

Bao la Green Rhino ya kocha, Jackson Amas lilifunikwa kimiani na Kevin Kariuki naye Musa Muthuma alisawazishia Y. Achievers. ‘

‘Kusema tunashukuru vijana wetu kwa kazi nzuri waliofaanya kwenye mashindano hayo ambapo kwa mara ya kwanza tulifanikiwa kubeba taji hilo kutoka Kinyago. Mara nyingi timu za eneo hilo hutulemea na kushinda mashindano mengi ambayo huandaliwa na shirika hilo pia katika Uwanja huo,” Kipkemoi wa Y.Achievers alisema na kuongeza kwamba KYSD ilifanya jambo nzuri kuandaa mashindano hayo hasa wakati huu wa jangaa la corona.

Alidokeza kuwa wakati huu vijana hawamo shuleni ambapo ni kipindi hatari sana kwao wasipopata jambo la kufanya mitaani. Katika mpango mzima timu za Kitui Village zimekuwa zikionyesha soka la nzuri ambapo wachezaji wazo wanahitaji kushikwa mkono maana tayari wameonyesha wanaweza kuibuka wanasoka watajika miaka ijayo.

Kwenye nusu fainali za kipute hicho, Y.Achievers iligonga A 1000 Street FC kwa magoli 5-1 kupitia Kelvin Kariuki na Feisal Mwangi mabao mawili kila mmoja huku Dennis Ndisi akitikisa wavu mara moja.

Naye Eliub Usiru alifungia A 1000 Sportiff bao la kufuta machozi. Kwenye nusu fainali ya pili, Green Rhino kupitia mipigo ya matuta iliangusha Wolves FC kwa mabao 2-1 baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

Kwenye mechi za robo fainali, Green Rhino ilinyanyua 3D FC, nayo Wolves FC ilishinda Godown Allstars kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoshana nguvu mabao 2-2 katika muda wa kawaida.

Nao chipukizi wa MASA walilala mbele ya Black Angels kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare tasa huku Young Achievers ililimwa na A 1000 Sportiff kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka mabao 2-2.

Mashindano hayo yalijumuisha jumla ya vikosi 20 ikiwamo: Young Achievers, Green Rhino, A 1000 Sportiff, Kinyago United, Black Jack FC, MASA, Volcano, LeMans, 3D FC, Godown Allstars, Wolves, Fearless FC, Black Angels, Etiquettes FC, E-Naisher, MJL, Tico Raiders na Locomotive FC.