Michezo

Young Dragon Karate Club yazidi kujituma

March 2nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

UNAPOFIKA katika ukumbi wa shule ya msingi ya Kenyatta mjini Thika, utawapata vijana chipukizi wa mchezo wa Karate ya Klabu ya Young Dragon Karate Club, chini ya kocha Elizabeth Rukwaro.

Anasema amewanoa chipukizi hao kwa miaka kumi tangu 2009 katika mtaa wa Makongeni Thika.

“Vijana wengi ninaonoa ni kati ya miaka 5 hadi 14 na wengi wao wanatoka katika familia maskini. Nilifikiria hivyo ili nibadilishe tabia zao. Mchezo wa Wakarate ni wa kudumisha nidhamu,” alisema kocha Rukwaro.

Alisema wengi wa chipukizi hao wanatoka katika mitaa ya mabanda kama Kiandutu, Umoja, Athena, na Matharau.

“Mimi mwenyewe huenda hadi vijiji hivyo na kuzungumzia na wakazi wa chipukizi hao baadaye wazazi hao hunikubalia kuwapeleka wana wao kwa mazoezi,” alisema  kocha Rukwaro.

Alisema vijana hao ambao ni wavulana na wasichana walisafiri hadi India mwezi February kwa mashindano ya dunia ya karate.

Alieleza kuwa waliweza kusafiri na vijana 12 ambapo walirejea na medali 34 huku wakiwa kwenye nafasi ya kwanza kati ya timu 11 zilizoshiriki. Medalist hizo ni dhahabu, fedha na shaba.

Baadhi ya wahisani walijitolea kununua tikiti za ndege kwa vijana hao.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina alinunua tikiti Tatu. Zingine zilifadhiliwa na kabisa na Kaunti ya Kiambu.

Anasema kile kinachoponza juhudi zake za kupiga hatua zaidi ni ukosefu wa Hela.

“Mimi kama mtu aliyeajiriwa, hutumia fedha zangu kuwafadhili baadhi ya vijana hawa.Kwa hivyo natoa mwito kwa wahisani popote walipo wajitolee ili kunipiga jeki  ili niwainue chipukizi hawa katika kiwango kingine cha kujivunia,” alisema kocha Rukwaro.

Alisema kila Mara anawahimiza vijana hao kujizatiti katika masomo yao ili kupata elimu na pia kuwa stadium katika mchezo.

Kocha huyo anaeleza kuwa amecheza karate kwa zaidi ya miaka 12 huku akijivunia ukanda mweusi wa 3rd Dan.

“Nimewahi kucheza timu ya wanawake kwa kiwango cha kitaifa huku nikisafiri nchi kadha za Ulimwenguni,” alifafanua Rukwaro.

Alitoa mwito kwa wanawake ambao wangetaka kupokea mafunzo ya kujikinga kutoka uvamizi ya ubakaji, wafike katika ukumbi wa Kenyatta, Makongeni, ili wapokee mafunzo maalum.

“Mimi kama mwana karate aliye na ujuzi nimefunza wanawake wengi ambao wako tayari kujikinga kutoka kwa maadui mwanaume,” alisema Rukwaro.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Kennedy Waimeri Ndaiga alitoa mwito kwa wahisani popote walipo wajitokeze ili kupiga jeki klabu hiyo.

“Sisi kama klabu tumejitahidi sana kuona ya kwamba vijana wetu wanakuwa watu wa kutegemwa katika siku za baadaye.

Alitoa mwito kwa wizara ya elimu nchini kuzingatia michezo zingine kama ajua,netiboli, ndondi,na raga.

Alisema vijana hao wanajiandaa kusafiri nchi kadha kwa muda wa miezi michache zijazo.

Baadhi ya nchi wanazojiandaa kuzuru ni Burundi, Afrika Kusini, na Uingereza.

“Wakati huu ndiyo tunatoa mwito kwa wahisani, na hata wafanyi biashara kujitokeza na kutoa chochote walicho nacho ili kuwapiga jeki kwa maandalizi hayo,” alisema Ndaiga.

Aliwapongeza vijana hao kwa kuonyesha bidii ya mchwa kwa sababu huwa hawachelewi kufika mazoezi ya kila siku kutoka Jumatatu hadi Ijumaa kutoka saa 11 za jioni hadi saa moja za jioni.