Michezo

Young Elephant yaicharaza Arizen

November 18th, 2020 1 min read

Na JOHN KIMWERE

YOUNG Elephant FC imelaza Arizen Soccer Academy kwa mabao 7-0 na kuendelea kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wao katika Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 12 muhula huu.

Elephant ya kocha, Jackson Amas ingali kileleni kwa alama 15 baada ya kushinda mechi zote tano ambazo imecheza. Nayo bingwa mtetezi Kinyago United ilisajili ushindi wa bao 1-0 mbele ya Blue Bentos na kutua nafasi ya sita kwa alama kumi.

Wafungaji wa Elephant walikuwa Duncan Njoroge na Musa Mutuma kila mmoja alipiga ‘hat trick,’ naye Dickson Ongola alitupia kimiani bao moja. ”Nashukuru wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliofanya na bila shaka tunalenga kuendeleza mtindo huo wa kugawa dozi dhidi ya wapinzani wetu,” kocha wa Elephant alisema.

Naye nahodha wa Kinyago, Abdallah Shame alipiga kombora moja na kubeba kikosi hicho kuvuna alama tatu muhimu. Nao chipukizi wa Tico Raiders waliona giza walipokanyangwa kwa mabao 9-2 na Pro Soccer Foundation.

Kwenye matokeo mengine, Biira Sports Academy ilinyuka Full Time Rangers mabao 4-0, A 1000 Sportiff ilipigwa mabao 2-1 na KYSA, Fearl ilizoa mabao 4-2 mbele ya Locomotive FC. Nazo Reggae Boys 1-1 Young Lions, SAFA 2-2 Sharp Boys nayo MASA ilitoka sare tasa dhidi ya Gravo Legends.

Katika jedwali la kinyang’anyiro hicho, Young Elephant inaongoza kwa kuandika alama 15, tatu mbele ya Pro Soccer Foundation sawa na KYSA tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nne bora inafungwa na Young Lions kwa alama 11 sawa na Fearl FC.