Michezo

Young Elephant yapania kushiriki Elite League msimu ujao

September 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Young Elephant ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 12 ni kati ya vikosi vinavyolenga kushiriki kampeni za michuano ya Elite League kwa wasiozidi umri wa 15 muhula ujao ambayo huandaliwa na Shirikishiko la Soka la Kenya (FKF) muhula ujao.

Kocha wa kikosi hicho, Jackson Amas anasema kwamba wamejiwekea malengo ya kushiriki mechi za kipute hicho msimu ujao ili kusaidia wachezaji hao kupiga hatua.

”Tunalenga kuanza kushiriki mechi hizo ili kunoa vipaji vya chipukizi wetu pia kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kutambuliwa ,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo pia itawezesha baadhi yao kuteuliwa katika timu za taifa za wachezaji wa umri wa chini.

Hatua hiyo itawapa nafasi kuonekana na maskauti na kuteuliwa kujiunga na timu za taifa hasa kwa wachezaji wa U-15, U-17 na U-20.

Young Elephant ina vikosi kadhaa vya wachezaji wenye umri tofauti kuanzia tisa hadi 18 (U-9, U-10, U-11, U-12, U-13, U-15, U-16 na U-18) ambazo hufanyia mazoezi katika Uwanja wa Majengo karibu na Kitui Village. Kadhalika wana timu moja ya wasichana ya wasiozidi umri wa miaka 14.

”Tulianzisha Young Elephant mwaka 2015 kwa malengo ya kusaidia wachezaji chipukizi kutambua talanta zao katika mchezo wa soka pia kwenye juhudi za kuwasaidia kujiepusha dhidi ya makundi ya uhalifu mitaani,” akasema na kuongeza kwamba timu za michezo mbali mbali zimesaidia wachezaji wengi tu katika eneo bunge la Kamukunji.

Kikosi hicho kinajivunia kushinda mataji tofauti katika mchezo huo. Mapema mwezi huu vijana hao walimaliza katika nafasi ya pili kwenye mechiza kuwania taji la KYSD walipolala kwa mabao 2-1 mbele ya Young Achievers katika fainali. Kwa jumla kocha huyo anasema kikosi hicho kinajivunia vikombe saba ambavyo kimeshinda kwenye mashindano mbali mbali tangia kianzishwe.

Chipukizi hao wanajivunia kushinda taji la Centre Eastleigh walipolaza Pro Legends FC katika fainali. Pia waliibuka mabingwa kwenye mashindano ya Shauri Moyo Youth, Pastor Jeremiah Tournament pia Vijana na Talanta.

Kadhalika chipukizi hao wameshiriki mashindano mengine kama:Peace Tournament, Malezi Tournament, Pumwani Group Red Cross Tournament, KYSD Laegue na St Johns League.

Young Elephant kwa wasiozidi umri wa miaka 12 inajumuisha wachezaji kama: Peter Morgan, John Aron, Musa Mutuma, Duncan Njoroge, Dickson Songola, Tobias Ochola, Khalid Musa, Duncan Onguong. Kocha huyo husaidiana na naibu wake Issa Juma.