Habari Mseto

ZABUNI: Yabainika afisa mkuu alialika EACC ikague mfumo

September 27th, 2020 2 min read

Na WANJOHI GITHAE

IMEBAINIKA kwamba Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kusambaza Dawa (Kemsa), Dkt Jonah Manjari, ambaye alisimamishwa kazi, alikuwa ameandikia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), akitaka msaada wa ukaguzi wa mfumo wa utoaji zabuni wa kampuni hiyo.

Dkt Manjari ambaye alisimamishwa kazi mwezi mmoja baada ya Kemsa kuzingirwa na ufisadi, inadaiwa alihofia baadhi ya wakora katika kampuni hiyo hawakuwa na nia njema na mpango wa utoaji huduma za afya bora kwa gharama nafuu.

Mpango huo ni kati ya ajenda anazotarajia kutimiza Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kustaafu mnamo 2022.

Ufichuzi huu umebainika wakati ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ( DPP), Bw Noordin Haji, anapanga kuamua iwapo atawashtaki mameneja wakuu kwenye kampuni ya Kemsa.

“Ni ombi langu kwamba tushirikiane na EACC kukagua mfumo wetu wa utoaji zabuni na kutambua hatari iliyoko ambayo inaweza kutoa mwanya kwa wizi kutokea,” Dkt Manjari alieleza EACC kupitia barua iliyoandikwa Julai 19, 2018.

Dkt Manjari aliteuliwa mkuu wa KEMSA mnamo Julai 1, 2018, kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mwezi uliopita, bodi ya wakurugenzi wa Kemsa iliamua kumsimamisha kazi Dkt Manjari pamoja na wakurugenzi wa idara ya mauzo na utoaji zabuni Eliud Muriithi na Charles Juma mtawalia.

Taifa Leo ilichapisha taarifa zilizoonyesha jinsi utoaji zabuni ulijaa mapendeleo na ufisadi huku baadhi ya kampuni ambazo zilisajiliwa miezi minne awali zikipewa kandarasi za kusambaza magwanda ya PPEs na vifaa vingine vya mabilioni ya fedha.

Kemsa ilitoa kandarasi kwa kampuni mbili, tenda iliy okuwa na thamani ya Sh3 bilioni za kuwasilisha bidhaa na vifaa vya kimatibabu ambavyo havikuwa kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha 2019/20 kufikia Juni 4.

Marafiki

Baadhi ya zabuni za mamilioni ya fedha zilitolewa kwa marafiki na watu wenye hadhi serikalini.

Vilevile kulikuwa na kandarasi ya Sh4 bilioni ambayo ilitolewa kwa kampuni moja iliyopendekezwa na mwanasiasa mashuhuri wa Jubilee.

Wiki mbili zilizopita, EACC iliwasilisha faili za uchunguzi kwa afisi ya DPP ili wahusika washtakiwe mahakamani.

“Nimechagua kikosi cha viongozi wa mashtaka ambao wana uzoefu na ufahamu mpana wa masuala ya kisheria kuchunguza faili hizo na kuwasilisha matokeo kwangu,” akasema Bw Haji kwenye taarifa yake.

Msemaji wa EACC, Bw Yasin Amaro, hata hivyo, alifichua kwamba tume hiyo hupokea maelfu ya maombi ya mifumo yao kukaguliwa, na akaongeza kuwa Wizara ya Afya ilikuwa imewasilisha ombi hilo mnamo 2018.

Mnamo Agosti 2018, EACC iliwasilisha kwa wizara ya afya ripoti iliyoangazia uimarishaji wa sera na mifumo yake ya kuweka bei za dawa na vifaa vya kimatibabu vilivyokuwa vikiwasilishwa nchini.

Ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Afya, Bi Sicily Kariuki na mwenyekiti wa EACC, Dkt Eliud Wabukala.

Ripoti hiyo ilionyesha udhaifu katika mifumo ya utoaji wa zabuni na pia katika usambazaji wa dawa na vifaa vingine vya kimatibabu katika sekta ya umma.

Kuhusiana na uongozi, EACC ilibaini kwamba hakukuwa na orodha ya wasambazaji wa dawa na vifaa vya kimatibabu ambayo iliidhinishwa na serikali.