Habari Mseto

Zabuni za kujenga Konza City zatangazwa kwa umma

August 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imetangaza zabuni za kujenga jiji la kisasa, Konza Techno City, miaka kadha baada ya mradi huo kuzinduliwa rasmi na aliyekuwa rais Mwai Kibaki, kabla ya kumaliza awamu yake.

Katika muda wa miaka mitano iliyopita, serikali imekuwa ikiwavutia wawekezaji katika ukuzaji wa jiji hilo lililo katika kaunti za Makueni na Machakos.

Kulingana na Mamlaka ya Ukuzaji wa Jiji la Konza ambayo inasimamia ukuzaji wa jiji hilo, inalenga wawekezaji kununua ardhi kukuza sekta sita ambayo ni pamoja na teknolojia, elimu, vituo vya kibiashara, maeneo ya makazi, mahoteli, bustani, viwanda na vituo vya kuuza mafuta.

Mamlaka hiyo ilisema hivyo katika tangazo la kibiashara, ambapo wawekezaji wana hadi Juni 30, 2019 kutuma maombi.

Awamu ya kwanza ya Jiji hilo bado inaendelea kujengwa, alisema Mkurugenzi Mkuu John Tanui katika tangazo hilo.

Ujenzi wake unatarajiwa kuchukua Sh80 bilioni. Mnamo 2017, kampuni ya Italia ilipewa kandarasi ya Sh40 bilioni kukuza disaini ya muundo msingi na ujenzi wake.