Habari za Kitaifa

Zack Kinuthia ahisi Lizzie Wanyoike alihitaji kuzikwa kiserikali

January 25th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara ya Elimu Zack Kinuthia mnamo Jumanne alilalamika kwamba serikali ilisusia mazishi ya mwekezaji mashuhuri Lizzie Muthoni Wanyoike aliyezikwa katika Kaunti ya Murang’a.

Bw Kinuthia alisema kwamba “ingekuwa ni serikali ile yetu ya Uhuru Kenyatta, yeye mwenyewe kama kiongozi wa taifa angeamrisha mazishi hayo ya Januari 23, 2024, yashirikishwe na Wizara ya Elimu”.

Alisema Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alikuwa na heshima kwa mashujaa wa nchi na ndiyo sababu alikuwa akihudhuria hafla za wawekezaji na hata wanamuziki.

“Licha ya marehemu Lizzie kufahamika kama mwekezaji wa kibinafsi wa kiwango cha juu zaidi katika taasisi ya kiufundi ambapo kila mwaka huachilia wahitimu zaidi ya 4,000, hakuna afisa wa serikali aliyefika katika mazishi yake,” akadai Bw Kinuthia.

Taifa Leo ilifichuliwa kwamba Naibu Rais Rigathi Gachagua akiandamana na maafisa wengine angehudhuria mazishi hayo yaliyofanyika katika eneo bunge la Gatanga.

Lakini hakujitokeza dakika za mwisho bila sababu kutolewa japo mmoja wa maafisa wake wa itifaki alidai “bahari ya kisiasa imechafuka Murang’a”. Alikuwa akirejelea uhasama wa Bw Gachagua na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Badala yake, Bw Gachagua aliandaa mkutano wa kujidhibiti kisiasa na madiwani wa Kaunti ya Nyandarua.

Viongozi waliofika katika mazishi hayo ni pamoja na Gavana Irungu Kang’ata, Naibu wake Bw Stephen Munania, waliokuwa wabunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth, David Murathe na Nduati Ngugi.

Mume wa Bi Lizzie Wanyoike alihudumu kama mbunge wa Gatanga kati ya 1992 na 1997 akifahamika kama Bw Mburu Wanyoike, kwa sasa pia akiwa marehemu.

Wengine walikuwa mbunge wa sasa wa Gatanga Bw Muriu, mbunge maalum Bi Sabina Chege, mbunge wa Roysambu Bw Waihenya Ndurangu na Seneta Nyutu.