Michezo

Zaha sasa ataka Palace wamwachilie ajiunge na Everton

September 13th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI mahiri wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ivory Coast, Wilfried Zaha, amewataka waajiri wake wa sasa wamwachilie ili ajiunge na Everton ambao wamefichua azma ya kumsajili.

Kocha Roy Hodgson wa Palace amethibitisha kwamba nyota huyo wa zamani wa Manchester United tayari amewasilisha ombi la kutaka kujiengua ugani Selhurst Park kufikia Oktoba 5, 2020, ambayo ni siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji.

Zaha, 27, alifunga bao la pekee lililowasaidia Palace kuwalaza Southampton 1-0 katika mchuano wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita wa 2019-20, Zaha alikuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kusajiliwa na Arsenal ambao badala yake walishawishika kumtwaa nyota Nicolas Pepe wa Ivory Coast.

Kushindikana kwa uhamisho wa Zaha hadi Arsenal ni jambo ambalo kocha Hodgson alisema kwamba liliathiri pakubwa matokeo ya mchezaji huyo msimu uliopita wa 2019-20.

“Zaha hajatulia tangu uhamisho hadi Arsenal utibuke. Hata hivyo, tunajitahidi kumsadikisha aendelee kuwa mchezaji wetu. Tusubiri tuone yatakayotokea kati ya sasa na Oktoba 5,” akasema Hodgson ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza.