Habari za Kitaifa

Zaidi ya 10 waangamia katika ajali mbaya barabara ya Kitui-Machakos

February 26th, 2024 1 min read

Na KITAVI MUTUA

ZAIDI ya abiria 10 wamefariki papo hapo na wengine wengi kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Katangi, Kaunti ya Machakos.

Basi hilo ambalo lilikuwa linasafiri kutoka Zombe Market, Kitui Mashariki likielekea Nairobi lilipoteza mwelekeo wakati lililopokuwa linachanja kona huku likishuka kuelekea Athi River, ambapo lilibingiria mara kadhaa.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Machakos Patrick Lobolia, waokoaji wa kwanza kwenye eneo la ajali waliopoa miili nane kutoka kwa gari hilo lililoharibika vibaya, huku watatu zaidi wakipoteza maisha yao wakiwa njiani kukimbizwa hospitalini.

Bw Lobolia aliambia Taifa Leo kwamba ajali hiyo ilitokea saa kumi na moja unusu jioni.

“Inaonekana kwamba dereva wa gari hilo alishindwa kudhibiti matatu hiyo kwenye sehemu hiyo ya mteremko kuelekea kwa mto,” alisema.

Kamanda huyo wa polisi alisema pindi gari hilo lilipopoteza mwelekeo, lilibingiria mara kadhaa na karibu litue ndani ya Mto Athi.

“Tumetuma vikosi vya uokoaji, ikiwemo ambulansi kukimbiza waliojeruhiwa hospitali zilizo karibu na Kitui na Machakos,” akasema.