Habari Mseto

Zaidi ya kesi 3,000 kuamuliwa siku 14 zijazo

April 3rd, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

ZAIDI ya kesi 3000 zitaamuliwa katika muda wa siku 14 zijazo huku Mahakama ikikumbatia teknolojia kuepuka msongamano wa watu wakati huu kuna hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Aidha, imesimamisha vibali vyote na maagizo ya kuwakamata washukiwa yaliyotolewa kufikia Machi 15, mwaka huu.

Hatua hii imesaidia kupunguza msongamano wa washukiwa na wafungwa katika magereza maambukizi ya virusi hivi yakiendelea kuongezeka nchini.

Kabla ya huduma kupunguzwa na maafisa wa Mahakama kuagizwa kufanya kazi kutoka nyumbani, majaji walikuwa wakichukua muda mrefu kuamua kesi huku washukiwa wakiteseka rumande.

Jaji Mkuu David Maraga alisema kwamba, shughuli ya kutoa maamuzi katika kesi inaendelea vyema katika mahakama zote nchini wakati huu majaji na Mahakimu wengi wanafanyakazi wakiwa nyumbani.

“Majaji wametumia fursa hii kuandika hukumu ya kesi walizokuwa wamekamilisha na wanaendelea kutoa maamuzi na hukumu kwa njia ya elektroniki,” alisema Bw Maraga baada ya kufanya mkutano kwa njia ya kidijitali na wakuu wengine wa mashirika yanayohusika na utekelezaji wa haki nchini.

Kufikia jana, kesi 2000 zilikuwa zimeamuliwa kwa njia ya kielektroniki na maelfu ya wafungwa, hasa wa makosa madogo kuachiliwa huru. Jaji Maraga alisema mfumo huu umefaulu na kesi 1779 zilishughulikiwa katika muda wa wiki moja.

“Tuna furaha kutangaza kuwa, katika muda wa wiki mbili zijazo, Mahakama ya Juu itatoa hukumu katika kesi moja na maamuzi ya kesi nyingine kumi,” Bw Maraga alisema.

Katika kipindi hicho, Mahakama ya Rufaa inatarajiwa kutoa maamuzi katika kesi 45 zilizowasilishwa Mombasa, Nairobi, Kisumu na Eldoret.

Kesi 369 zitaamuliwa katika Mahakama Kuu na nyingine 269 katika Mahakama ya kushughulikia mizozo ya ardhi. Kesi 400 zitaamuliwa katika Mahakama za Mahakimu na kadhi kote nchini katika kipindi hicho.

“Majaji na Mahakimu wataendelea kutumia kipindi hiki wanachofanya kazi wakiwa nyumbani kuandika maamuzi katika kesi walizokuwa wamesikiliza. Orodha ya hukumu zilizotayari itakuwa ikichapishwa katika tovuti za Mahakama, chama cha wanasheria na Shirika la masuala ya sheria nchini, Kenya Law Reports,” alisema Bw Maraga.

Katika kesi za uhalifu, majaji na mahakimu wamekuwa wakisoma hukumu za wafungwa walio rumande kwa njia ya kielektroniki huku wakifahamisha mawakili wa pande zote katika kesi za kijamii na ardhi kwa njia ya baruapepe kuhusu maamuzi ya kesi zao.

Jaji Maraga aliagiza polisi, madalali na maafisa wote wanaotekeleza maagizo ya Mahakama kutotekeleza vibali na maagizo yote yaliyotolewa kabla ya Machi 15, 2020.