Habari Mseto

Zaidi ya vyama 400 kumenyania kura za 2022

October 1st, 2020 1 min read

Na David Mwere

ZAIDI ya vyama 400 vipya vya kisiasa vimetuma maombi ya kusajiliwa.Idadi hiyo kubwa huenda ikaashiria wanasiasa wanajipanga na kuweka mikakati ya mapema kwa kinyang’anyiro cha 2022.

Ofisi ya msajili wa vyama vya kisiasa imepokea jumla ya maombi 405 ya kusajili vyama vipya vya kisiasa miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Rekodi katika ofisi hiyo zinaonyesha kuwa tayari kuna vyama 83 vilivyokuwa vimesajiliwa nchini kufikia Jumatatu iliyopita na vingine saba vinavyosubiri usajili rasmi.

Vyama saba vinavyosubiri kusajiliwa rasmi ni Kenya Moja People’s Party (KMPP), African Development Congress (ADC), Umoja Summit Party (USP), National Reconstruction Alliance (NRA), Party for Growth and Prosperity (PGP), Entrust Pioneer Political Party (EPPP) and Party for Peace and Democracy (PPD).

Mtaalamu wa masuala ya utawala Barasa Nyukuri anasema huenda wanaosajili vyama wanalenga kunufaika kwa pesa kutoka kwa wawaniaji, hasa watakaokosa tikiti kwa vyama walivyomo sasa.