Habari Mseto

Zaidi ya Wakenya 2,000 sasa wanaugua Covid-19

June 1st, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya watu walioambukizwa Covid-19 Jumatatu ilivuka watu wa 2,000 baada ya watu 59 wapya kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Waziri ya Afya Mutahi Kagwe, idadi jumla ya visa nchini Kenya sasa ni 2,021.

Wagonjwa wanane waliruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kupona, na kufikisha idadi ya waliopona kufikia Jumatatu kwua 485.

“Wakati huo huo, wagonjwa watano walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na Covid-19. Hii inafikisha idadi ya waliofariki kuwa 69,” Bw Kagwe akasema.

Kulingana na idadi ya visa vipya vya maambukizi, Nairobi iliandikisha viaa 29, Mombasa (14), Turkana (6), Busia (4), Taita Taveta (2), Kajiado (2) huku Kiambu na Kilifi zikiandikisha kisa kimoja kila moja.

Katika kaunti ya Nairobi, visa vya maambukizi viligunduliwa kama ifuatavyo; Ruarajka visa vinane, Westlanda (6), Dagoreti Kaskazini (4), Langata (4), Kibra (3). Na maeneo bunge ya Kasarani, Kamukunji na Makadara zilirekodi kisa kimoja pekee.

Visa vyote vinane kutoka eneo bunge la Ruaraka vilipatika katika vituo vya karantini.

Katika kaunti ya Mombasa; eneo bunge la Mvita liliandikisha visa sita huku maeneobunge ya Jomvu na Changamwe yakiripoti visa viwili kila moja.