HabariKimataifa

Zambia kuwasukuma jela watakaonaswa wakiwa na 'Samantha'

March 12th, 2018 2 min read

NA AFP

LUSAKA, ZAMBIA

SERIKALI imeanzisha msako mkali dhidi ya madoli ya mahaba na kuonya kuwa watakaopatikana nayo wataadhibiwa kwa kufungwa gerezani.

Hatua hiyo imepelekea suala la madoli ya mahaba ligonge vichwa vya habari na kuibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii ambapo kuna misimamo tofauti katika nchi hiyo iliyo yenye misimamo ya kitamaduni na kidini kusini mwa Afrika.

“Kutokana na kuwa nchi hii ni ya Kikristo, ni wazi kwamba tunaongozwa na misingi ya Kikristo ambayo yanahusu maadili na tabia njema,” akasema Waziri wa Mwongozo wa Taifa na Masuala ya Kidini, Bi Godfridah Sumaili.

Kulingana naye, uuzaji au utumizi wa madoli ya mahaba ni kinyume cha sheria za Zambia. Aliapa kuwa serikali itahakikisha vidosho hao bandia hawatanunuliwa kupitia kwa intaneti wala kuingizwa nchini kutoka nchi za nje.

“Sheria inazuia mtu yeyote kufanya biashara au kutumia vidude aina hii kwa hivyo ndio maana tunaambia Wazambia kwamba hiki ni kitu ambacho si cha kawaida kabisa,” akasema.

Waziri huyo alisema marufuku iliyotolewa inastahili, baada ya vyumba vya habari kuripoti kuwa madoli hayo huingizwa nchini kutoka mataifa ya bara Asia. Alisema polisi wanachunguza madai hayo.

Kwa miezi kadhaa sasa, vyumba vya habari Zambia vimekuwa vikitenga sehemu nyingi magazetini kuchapisha habari na maoni kuhusu maduka ambayo yameanza kuongezeka katika mji mkuu wa Lusaka kuuza vidoli vya mahaba.

“Mungu aliumba mume na mke ili waridhishane kimahaba, lakini mwanamume au mwanamke anapoamua kutumia kiumbe kisicho na uhai hiyo ni tabia mbovu. Tusilete imani na tabia za kigeni humu nchini. Tushikilie tu imani zetu wenyewe,” akasema.

Watengenezaji wa vidoli vya mahaba husema wanaweza kutibu upweke na kusaidia wanaume wakongwe ambao hawana wake.

Chama cha Patriots for Economic Progress (PEP) nchini humo kilisema msimamo wa serikali kuhusu vidoli hivyo unaonyesha jinsi utawala wa Rais Edgar Lungu unazidi kuwa wa kiimla.

“Msimamo kuwa Biblia hairuhusu utumizi wa kidude chochote ni makosa,” akasema mkuu wa chama hicho, Sean Tembo.

Aliongeza: “Ni Biblia hiyo hiyo ambayo hupeana uhuru wa kuamua na itakuwa makosa kumfunga mtu gerezani kwa kuamua kutumia vidoli vya mahaba. Kuna wanaume ambao hawajiamini na hawaezi kutongoza.”