Habari za Kitaifa

Zamu ya wakulima kunyolewa kupitia ushuru  

February 25th, 2024 2 min read

NA BARNABAS BII

WAKULIMA sasa wataonja makali ya ulipaji ushuru kidijitali, baada ya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kuwataka watumie mfumo wa Kudhibiti Malipo ya Ushuru Kielektroniki (eTims).

Kupitia mfumo huo, KRA inalenga kukusanya mamilioni ya pesa zinazotokana na mapato ya mazao yao shambani.

Majuzi serikali ilitangaza kuwa kila mkulima sharti atozwe asilimia tano ya pesa ambazo ni sawa na thamani ya mauzo yake.

Hatua hii ni ya hivi punde zaidi baada ya maafisa wa KRA kuvamia vinyozi na wanaoendesha biashara za urembo.

Katika baadhi ya miji nchini, hata waendeshaji bodaboda wamejipata wakitozwa ushuru pamoja na ada za uegeshaji.

Aidha, baadhi ya wamiliki wa maduka ya vinyozi jijini Nairobi, walisema kwamba, wameandamwa na watu wa KRA na kutakiwa walipe ushuru wa mapato wa asilimia 16.

Nao wafanyikazi kwenye maduka hayo ya vinyozi wanatakiwa wakatwe asilimia tano ya mapato yao, kama sehemu ya ushuru kwa serikali.

Na sasa, KRA inawataka wakulima watumie mfumo wa eTims kutoa hesabu kuhusu mapato yao.

Lakini sasa, mwenyekiti wa chama cha wakulima nchini, Kipkorir arap Menjo analalama kuwa agizo hilo litawafinya wakulima, na kuwahangaisha wale walio mashambani.

“Mfumo huu unafanya kazi vyema kwa wakulima wa mijini na wasomi. Hao wana simu za kisasa. Lakini una madhara kwa wakulima wa mashambani ambao hawana simu au intaneti,” akasema Bw Menjo wakati wa mkutano uliofanyika Eldoret.

Gad Kamarei, mkulima katika Kaunti ya Laikipia akionyesha mazao ya nyanya kutoka shambani mwake. PICHA|SAMMY WAWERU

KRA tayari imewaelekeza wakulima kujisajili na eTims kwa kutumia simu zao au mfumo wa mtandaoni.

Kando na hayo, KRA imekuwa ikiendeleza uhamasishaji kuhusu jinsi mfumo huo unavyotumika.

Hazina ya Kitaifa inapanga kukata asilimia tano kama ushuru kwa mazao ya shambani yanayouzwa kwa vyama vya ushirika na wasindikaji.

Chini ya mfumo mpya wa biashara, wakulima wanatakiwa kutoa kodi ya kielektroniki kwa miamala yote wanayofanya.

Bila kufanya hivyo, hawawezi kudai malipo wakati wa kuwasilisha Kodi ya Mapato.

“Baadhi ya wakulima hawajasajiliwa chini ya vyama vya ushirika. Wanahitaji uhamasisho kabla ya mfumo mpya wa ushuru kutekelezwa,” alisema Jackson Kemboi kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Baadhi ya watu katika eneo la Magharibi mwa Kenya wameelezea hofu kwamba, huenda wakatozwa ushuru kwa malipo yanayofanywa kwa wakulima kwa ununuzi unaofanywa bila kutumia mfumo huo wa eTims.

Kulingana na KRA, mfumo huo mpya utaisaidia serikali kufuatilia mabadiliko ya hisa kwa biashara ndogo ndogo, haswa wakulima wanaosambaza bidhaa zao kwa vyama vya ushirika.

Ingawa wakulima hao wanalia, azma ya serikali kuhakikisha kila mtu na kila sekta inalipa ushuru inazidi kuimarika.

Wahudumu wa teksi kidijitali kama vile Uber, tayari wameanza kuwatoza madereva ushuru huo wa asilimia tano.

Kwa safari ya Sh1, 000, Uber inatoza Sh180 pamoja na ushuru wa Sh28.80.

Mswada kuhusu Nyumba za Bei Nafuu uliopitishwa bungeni Jumatano unaonyesha kuwa, Wakenya ambao hawajaajiriwa (mahasla) watatozwa asilimia 1.5 ya faida za biashara na shughuli zao sawa na wenzao walioajiriwa, ili kugharamia ujenzi wa nyumba hizo.