Zanu PF yashinda viti vingi bungeni huku fujo zikianza

Zanu PF yashinda viti vingi bungeni huku fujo zikianza

Na AFP

CHAMA tawala cha Zimbabwe, ZANU-PF, kilishinda viti vingi zaidi vya ubunge, matokeo rasmi yalionyesha Jumatano. 

Kura za urais zilikuwa zinaendelea kuhesabiwa huku chama pinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) kikilalamika kuhusu ulaghai katika uchaguzi huo wa kwanza tangu serikali ya aliyekuwa rais Robert Mugabe ilipopinduliwa baada ya kuongoza kwa miaka 37.

Wakati wa utawala wa Mugabe, chaguzi zilikumbwa na ulaghai na vita.

Rais Emmerson Mnangagwa, 75, ambaye alichukua mahala pake kwa muda, aliahidi uchaguzi huu ungekuwa huru na wa haki na akaalika waangalizi wa kimataifa kuushuhudia.

“Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC) imetangaza matokeo 50 zaidi ya ubunge, na hivyo basi kufikia sasa kuna matokeo ya viti 153. Miongoni mwa 153, ZANU-PF imeshinda viti 110 huku Muungano wa MDC ukipata viti 41,” shirika la habari la taifa la ZBC liliripoti.

Kwa jumla, kuna viti 210 katika bunge la taifa la chini.

Ingawa MDC haikuzungumzia matokeo hayo mara moja, kiongozi wa chama hicho Nelson Chamisa, 40, jana alisema matokeo ya kura za urais yanafanyiwa ulaghai.

“ZEC inataka kubadilisha uamuzi wa wananchi kuhusu kura za urais. Mpango huo umenuiwa kufanya wananchi wajiandae kukubali matokeo feki ya uchaguzi wa urais. Tulishinda uchaguzi huu na hatutakubali kuibiwa,” akasema kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Ikiwa hakuna mshindi atapata asilimia 50 za kura kwenye awamu ya kwanza ya uchaguzi, kutakuwa na awamu ya pili Septemba 8.

Wafuasi wa MDC walianza kusherehekea Jumanne baada ya afisa mkuu wa chama hicho kusema wana hakika Chamisa alishinda na ikiwa hatatangazwa mshindi, “watatangaza matokeo yao wenyewe”.

Tangazo hilo lilimpelekea Waziri wa Masuala ya Ndani Obert Mpofu, kuonya kwamba mtu yeyote atakayetangaza matokeo kiharamu atakabiliwa vikali kisheria na kutupwa gerezani.

Tume ya uchaguzi ilisema haitawezekana kutangaza matokeo ya kura za urais kabla kesho wala hata Jumamosi, na matokeo hayatatangazwa hadi hesabu zote zikusanywe kutoka vituo vote 10,985 vya uchaguzi.

Kisheria tume hiyo huwa imepewa siku tano kutangaza matokeo baada ya uchaguzi wa urais kufanywa.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Priscilla Chigumba, ambaye ni jaji wa mahakama kuu, alikanusha madai kwamba kulikuwa na mapendeleo na wizi wa kura katika uchaguzi huo.

You can share this post!

Utumizi wa Kiswahili shuleni wazua ubishi TZ

Walioingiza wasichana wa Nepal nchini kunengua viuno...

adminleo