Michezo

Zapata atasalia kuinoa Ingwe – Mule

August 1st, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa AFC Leopards Dan Mule amemhakikishia kocha Rodolfo Zapata uungwaji mkomo na kusisitiza kwamba klabu hiyo haina mpango wowote wa kutafuta huduma za mkufunzi mpya.

Mule alisikitika kwamba Ingwe wamewabadilisha makocha mara nne ndani ya kipindi cha miezi 17 na akaahidi kwamba mtindo huo lazima ufike kikomo ili kuhakikisha kikosi kinadumisha na kuendeleza udhabiti.

Akizungumza akionekana amehamaki, Mule alipuzilia mbali taarifa zilizochipuka mwisho wa Julai kwamba Ingwe huenda wakaagana na Mwaajentina huyo aliyelalamikia hujuma kutoka kwa benchi yake ya kiufundi anaodai wanatiwa fitina na baadhi ya wanachama wa baraza kuu la Ingwe(NEC) wasiofurahia kazi yake wala uwepo wake klabuni.

Hata hivyo, Mule alisimama kidete na kusema Zapata aliyepokezwa kazi hiyo Mei 2018 haendi popote jinsi walivyong’atuka watangulizi wake Dennis Kitambi, Robert Matano na Steward Hall.

“Swala la kutafuta huduma za kocha mwengine halifai hata kufikiriwa kwa sasa,” akasema Mule.