Makala

ZARAA: Mbinu maalum ya kuzuia usambaaji wa wadudu hatari

November 28th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

MBALI na kuwepo kwa bei duni ya mazao katika shughuli za kilimo, kero la wadudu na magonjwa pia ni miongoni mwa changamoto zinazozingira wakulima.

Hilo hasa linachochewa au kuchangiwa na gharama ya juu ya dawa kukabiliana na pandashuka hizo, ikiambatana na ile ya pembejeo kama vile mbegu na fatalaiza. Katika upanzi, baadhi ya wakulima wanakumbatia utumizi wa mboleahai yaani ya mifugo, ili kushusha gharama ya uzalishaji.

Dawa na fatalaiza zinaendelea kuwa ghali kila uchao, zingine zikiwa za hadhi ya chini, licha ya kilio cha wakulima.

Charles Mwangi ni mkulima wa mboga na matunda eneobunge la Mathira, lililoko Kaunti ya Nyeri. Bw Mwangi pia hukuza viazi, karoti, matunda na mahindi.

Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika uzalishaji wa kabichi, spinachi na sukumawiki. Ili kupunguza gharama ya ununuzi wa dawa, mkulima huyo ameibuka na mbinu ya kipekee kuzuia usambaaji wa wadudu na magonjwa.

Upandaji wa mahindi kandokando mwa anachokuza, hata ingawa si asilimia mia kwa mia, Mwangi anasema unasaidia pakubwa kupunguza usambaaji hususan wa wadudu. “Kwa muda ambao nimekumbatia mfumo huu, kero la wadudu na magonjwa limepungua pakubwa ikilinganishwa na hapo awali,” adokeza mkulima huyo.

Aghalabu, usambaaji wa wadudu na magonjwa unachangiwa na upepo, na kulingana na mkulima huyo kasi yake (upepo) inadhibitiwa kwa kuzingira mimea kwa upanzi wa mahindi kandokando.

Katika kila zao, Mwangi amegawanya shamba lake kwa makundi ya mpangilio huo. Wakati wa ziara ya Akilimali, tulimpata akiwa na mboga aina ya spinachi na matundadamu maarufu kama tree tomato.

“Kuna magonjwa yanayosambazwa na upepo, hivyo basi kwa mpangilio huu ninapambana na yaliyoko udongoni pamoja na wadudu wanaojificha humo,” akaelezea.

Isitoshe, mfumo huo kulingana na wajuzi wa masuala ya kilimo unasaidia kukabiliana na suala la mmomonyoko wa udongo hasa msimu wa mvua. “Mvua kubwa ikinyea, ni rahisi kusomba udongo na mboga kama vile spinachi, sukumawiki na kabichi na hata za kienyeji kwa kuwa mizizi yake si dhabiti. Mahindi yakipandwa pembezoni, mihindi iwe karibu na mashina yake kuwekwa majani, kasi ya maji itadhibitiwa na mkondo wake kuelekezwa kwingine,” afafanua Njeri Murage, mtaalamu.

Hata hivyo, mdau huyo anasema kuwa mpangilio huo haukabiliana na athari za wadudu na magonjwa si hakikisho kuwa changamoto hizo zinatatuliwa kikamilifu.

“Haimaanishi mkulima ataepuka wadudu na magonjwa yaliyomo shambani. Ni njia tu ya kujaribu kupunguza kasi ya upepo mkali, usambaaji wa baadhi ya wadudu na magonjwa, sawa na inavyochukuliwa katika kilimo cha mahema (greenhouse),” asema Bi Njeri.

Mfumo huo kwa Kiingereza border cropping unafanya vyema katika ukuzaji wa mboga, matunda, karoti na hata maharagwe. Umechukua mahala pa matuta (terraces).

Njeri anaiambia Akilimali kuwa badala ya wadudu kushambulia mimea na mazao, watavutiwa na mahindi. “Mimea inayopandwa kandokando au kwenye mipaka, inapaswa kuwa mirefu kuliko inayozuiwa,” asisitiza.

Mbali na mahindi, mkulima anaweza kupanda nyasi aina ya mabingobingo (Napier grass). Ni nyasi zenye mashina magumu, na hurefuka hadi kimo cha mita nne.

Aidha, majani yake huwa na upana wa karibu sentimita nne na urefu wa sentimita 110, maumbile yanayosaidia kupunguza kasi ya upepo na ni kipenzi cha wadudu. Kwa wafugaji wa ng’ombe, ni zao linalosifiwa kusheheni madini kuntu. “Nyasi za mabingobingo hasa zikiwa mbichi zinapendwa sana na wadudu. Mkulima akizipanda kandokando mwa shamba lake au kwenye matuta, kando na kuwa chakula cha mifugo ni makazi ya wadudu,” aeleza Njeri.

Mtaalamu huyo pia anafafanua kuhusu mbinu ya “push and pull”, ambapo mahindi, mimea inayoorodheshwa katika familia ya legumi kama vile maharagwe, pamoja na nyasi aina ya mabingobingo, yote yanapandwa kando kando mwa shamba au kwenye matuta ili kunasa wadudu kwa njia ya kuwavutia. “Siri nyingine, kwenye matuta hayo mkulima apande vitunguu. Wadudu hawapendi harufu ya zao hilo,” afichua mdau huyo.

Katika shamba la Bw Mwangi, lenye ukubwa zaidi ya ekari mbili, robo ameipamba kwa spinachi na sehemu nyingine matundadamu. Kila kipande kimegawanywa na kuzingirwa kwa mahindi yailyoko kandokando na katika matuta.

“Kando na kupata mazao ya ninachokuza, huvuna mahindi ambayo pia yana mapato pamoja na kuwa lishe kwa familia yangu,” anasema Charles Mwangi.