ZARAA: Uundaji bidhaa za avokado kusaidia kupanua soko lake

ZARAA: Uundaji bidhaa za avokado kusaidia kupanua soko lake

NA SAMMY WAWERU

MAPARACHICHI ni kati ya matunda ambayo kwa sasa yana soko lenye ushindani mkuu, ikilinganishwa na miaka ya awali.

Maarufu kama avokado, yana thamani hasa katika masoko ya ng’ambo. Nchi za Bara Uropa, Uingereza, Milki za Kiarabu (UAE), Urusi na China, ndio wanunuzi wakuu wa mazao ya Kenya.

Ripoti ya Taasisi ya Unakili wa Takwimu Nchini (KNBS) mwaka 2021, imeonyesha maparachichi yaliyouzwa katika masoko hayo yaliingiza mapato ya Sh14.6 bilioni. Kulingana na mashirika yanayokusanya mazao ya wakulima waliopewa kandarasi na kuyatafutia wateja, yaliyoongezwa thamani yana soko la haraka.

Kongamano la Chama cha Ushirika cha Kitaifa cha Wazalishaji wa Avokado (ASOK), lililofanyika Juni, jijini Nairobi, lilijadili pakubwa kuhusu soko la zao hilo, huku mdahalo mkuu ukiangazia maparachichi yaliyosindikwa. Kongamano hilo lilihimiza wakulima kukumbatia mfumo huo wa uongezeaji thamani ili kuboresha mapato yao.

Peru, Mexico na Australia, ni mataifa yanayoongoza ulimwenguni katika uzalishaji, na yamevalia njuga uongezaji thamani. Nchi hizo, zimezindua viwanda vya kutengeneza mafuta ya maparachichi ambayo ni mithili ya mahamri moto sokoni.

Kongamano hilo likiwa makala ya kwanza ya ASOK kuleta pamoja wanunuzi, wakulima na wadauhusika kutoka sekta ya serikali na kibinafsi, pia lilishirikisha baadhi ya kampuni nchini zinazouza matunda hayo ng’ambo.

William Magoma (kulia), afisa kutoka Olivado na mwenzake Joseph Kairu, wakionyesha mafuta ya avokado yaliyotengenezwa na kampuni hiyo, katika kongamano la ASOK, jijini Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Ikiwa na makao yake Sagana, Murang’a, Olivado EPZ Ltd imekuwa ikizalisha avokado kwa zaidi ya miaka kumi. Katika hema lake, ilionyesha avokado, miche na mafuta yatokanayo na matunda hayo.

“Hata ingawa hatukuzi matunda yenyewe, tuna kandarasi na wakulima wanatusambazia mazao kuwatafutia soko ughaibuni,” akasema William Magoma, afisa kutoka Olivado.

Ina jumla ya wakulima 3,000, Magoma akidokeza, muhimu ni mkulima kuwa na angalau miti mitatu ya avokado, kuthibitisha umiliki wa shamba na kukubali kushirikiana nayo. Olivado ina soko tayari Ufaransa, Uholanzi na New Zealand, kwa mwaka ikikusanya zaidi ya 3 milioni kutoka kwa wakulima.

Hali kadhalika, huzalisha miche iliyoimarishwa ya Hass, ikiendeleza huduma zake kwa wakulima kuwashauri mbinu bora na mifumo ya kilimo endelevu.

“Kwa sababu ya athari za tabianchi kwa mazingira, tumeibuka na miche inayostahimili kero ya wadudu, magonjwa na kiangazi,” Magoma anaiambia Akilimali.

Isitoshe, kampuni hiyo imejiunga na mtandao wa uongezaji avokado thamani ikilenga matunda yanayokataliwa. Ina kiwanda eneo la Mirira, Sagana, ambapo huunda mafuta.

“Tani moja inazalisha karibu lita 100, na kwa siku hukama tani 40,” mtaalamu huyo aelezea, akidokeza kwamba robo lita ya mafuta ya maparachichi haipungui Sh1,000.

Keitt Exporters Ltd, ni kampuni nyingine inayotafutia wakulima wa avokado wanunuzi ng’ambo. Meneja wa Mauzo, Grace Thuita alidokeza ina mashamba eneo la Embu, Meru na Subukia, mianya yake ya soko ikiwa Bara Uropa, UAE na Urusi – japo mgogoro unaoendelea Urusi umeharibu hesabu zake.

“Tuna zaidi ya wakulima 5,000 eneo la Kati na Eldoret, kila msimu tukilenga kuuza kontena 400 – 500,” anaelezea.

Kontena moja ina uzani wa tani 23, 000, Grace akifichua katoni ya avokado za kilo 4 huuzwa kati ya Sh380 – 400.

Isitoshe, imekumbatia mfumo wa uongezaji thamani, kutengeneza mafuta afisa huyo akiridhia teknolojia hiyo katika kuhakikisha hakuna tunda linalopotea.

Miaka mitatu iliyopita, serikali ya Kenya na China ilitia saini mkataba Kenya kuuza avokado zilizogandishwa nchini humo. Makubaliano hayo yalitathminiwa mapema mwaka huu na kujumuisha zile mbichi zilizokomaa, hivyo basi kupanua soko.

“Hivi karibuni tutapata mwanya mwingine wa soko, India,” afichua Afisa Mkuu Mtendaji, ASOK, Ernest Muthomi.

Takwimu za KNBS zinaonyesha, kwa mwaka Kenya huzalisha tani 500,000.

  • Tags

You can share this post!

BI TAIFA JULAI 06, 2022

TAHARIRI: Rais Uhuru na Ruto wakomeshe tofauti zao za...

T L