ZARAA: Vitafunio vya wimbi vyazua msisimko sokoni

ZARAA: Vitafunio vya wimbi vyazua msisimko sokoni

NA SAMMY WAWERU

PASILICA Wanyonyi amekuwa mkulima wa nafaka kwa muda mrefu, na ikiwa kuna changamoto kuu anayohoji inazingira wakulima ni kero ya soko inayochochewa na mabroka.

Ni mkuzaji mkuu wa wimbi na soya katika kijiji cha Okilidu, Busia. Pasilica pia ni mkulima wa mahindi.

Mwaka wa 2010, ulikuwa miongoni mwa ambayo mkulima huyu anataja alipitia changamoto za soko.

“Nilikuwa nimevuna magunia 10 ya wimbi niliyouza Sh3, 200 kila moja kupitia broka, mapato yalikuwa duni nikilinganisha na gharama ya uzalishaji,” asema.

Hukuza wimbi kwenye ekari tatu na nusu, soya nusu ekari na mahindi ekari moja.

Anasema mauzo yalikuwa kipindi ambacho mmoja wa wanawe alikuwa anajiunga na chuo kikuu, hivyo basi alihitaji pesa kwa hali na mali.

Pasilica anasema mambo yalianza kuimarika 2012, alipojiunga na The International Crops Research Institute for the Semi-Arid Tropics (ICRISAT).

Shirika hilo lisilo la kiserikali hupiga jeki wakulima maeneo jangwa na nusu jangwa nchini.

“Pamoja na wakulima wengine, tulijiunga kama kundi tukafunzwa mifumo ya kuongeza nafaka thamani,” Pasilica ambaye aliingilia shughuli za kilimo 2000, aelezea.

Aidha, alianza kulima wimbi kwenye ekari mbili.

Chini ya Kundi la Muhula Women’s lenye jumla idadi ya wanachama 10, Pasilica alipata ujuzi na maarifa ya kuoka vitafunio.

“Tulipitia programu kadhaa za mafunzo,” adokeza.

Isitoshe, kulingana na mkulima huyu, ICRISAT iliwasaidia kupata soko bora na lenye ushindani mkuu la mazao.

“Magunia 50 ya mazao ya wimbi niliyouza kama mbegu, nilipata faida ya Sh200, 000,” aelezea, akiridhia mipango ya shirika hilo.

Pasilica kwa sasa ni muokaji wa crackies – kripsi na mandazi.

Aidha, ana kampuni ya kuoka vitafunio hivyo anavyotengeneza kwa kutumia wimbi, inayojulikana kama Pawa Bakers.

Ana mashine zilizoboreshwa kutekeleza uokaji.

Mama huyu wa watoto watano ana soko tayari la bidhaa zake kwa taasisi kama vile shule Busia na maduka ya jumla na rejareja.

Hata hivyo, Pasilica anasema safari kufikia alipo haijakuwa mteremko.

Pasilica Wanyonyi mkulima wa wimbi na soya Busia akionyesha bidhaa alizoongeza thamani kwa kutumia unga wa wimbi. PICHA | SAMMY WAWERU

Alikuwa akichuuza bidhaa kutoka boma – nyumba moja hadi nyingine, nyakati zingine akilazimika kuuza kwa bei ya kutupa yaani hasara.

“Uongezaji thamani nafaka una mapato ya kuridhisha,” asisitiza.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu ICRISAT, Dkt Jacqueline Hughes wakulima katika maeneo ya jangwa na nusu-jangwa wanapaswa kukumbatia mifumo ya uongezaji thamani mazao ya shambani ili kuvuna mapato ya kuridhisha.

“Kama shirika linalopiga jeki wakulima maeneo kame, tutaendelea kuwahamasisha kuongeza mazao thamani,” Dkt Hughes asema.

Afisa huyo vilevile anahimiza haja ya kukumbatia mifumo ya kidijitali na teknolojia ya kisasa kuboresha shughuli za zaraa.

Kilo ya crackies, Pasilica huuza Sh200 huku kipakio cha mandazi 6 Sh50.

“Covid ilipotua nchini, biashara ilinoga kiasi cha kuunda faida mara dufu. Kwa sasa, gharama ya juu ya operesheni inatishia utendakazi hasa mfumko wa bei ya mafuta ya mapishi,” Pasilica asema, akihimiza serikali kutathmini suala hilo.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo atatiza kampeni za Sonko kwa kuhepa Raila

MITAMBO: ‘Mixer’ ya kuchanganya viungo kutoka...

T L