ZARAA: Wajukuu wanafurahia matunda ya bidii yake

ZARAA: Wajukuu wanafurahia matunda ya bidii yake

NA WYCLIFFE NYABERI

MJI wa Magena, unaopatikana eneobunge la Bomachoge Borabu, Kaunti ya Kisii, unafahamika vyema kwa ukuzaji wa mboga asili kama vile managu, saga na kunde.

Wakazi wengi hapa, hasa kina mama, wamejikita migundani kulima mboga hizo za kienyeji. Kila unapouzuru mji huo, utayaona malori makubwa yameegeshwa kando kando sokoni humo yakingoja mazao hayo yayasafirishe mijini.

Lakini mzee mmoja kwa jina Elijah Ogamba, 81, ameamua kwenda kinyume na wakulima wengine kwa kuzamia kilimo cha Gooseberries, ama matunda bukini tangu ujana wake.

Matunda hayo ambayo wengi hawajui kuwa yanalimwa kwa kuwa zamani yalikuwa yakipatikana msituni, ni kitega uchumi kikubwa kwa mzee huyu aliyekuwa chifu wa koo zima la Abamachoge wakati wa utawala wa mkoloni.

Safu ya Akilimali ilimtembelea mkulima huyo anayeishi kijijini Riomanga, karibu na mpaka wa jamii za Abagusii na Maasai huko Transmara ili atupambanulie mengi kuhusu kilimo hicho.

Mbali na kumsaidia kuwasomesha watoto wake 14, Ogamba alieleza kuwa chumvi nyingi aliyoila ni kutokana na afya nzuri anayoipata kwa kula matunda hayo kwa wingi.

Kwa kuwa umri wake mpevu hauwezi kumruhusu alime, yeye huwatumia watu kumlimia lakini kazi nyingine za upanzi na uchungaji wa mimea yake, anazifanya yeye.

“Nilifutwa kazi ya uchifu miaka ya sabini katika hali tatanishi. Siku moja nilipomtembelea binti yangu mjini Kisii, niliona mimea ya bukini nje ya nyumba yake na nilichuma baadhi ya matunda nikaja nayo nyumbani kutengeneza mbegu ambazo ndizo chimbuko la mimea hii yote mnayoiona hapa,” Omanga anasema.

Kilichomchochea zaidi Ogamba kukumbatia bukini, ni kwamba kila mara alipokuwa akienda mjini Kisii, jamii za Wahindi ambao wana maduka makubwa mjini huko, walikuwa wakiwauliza vijakazi wao wanakoweza kupata bukini.

“Kwa kuwa matunda ya bukini hayakuwa yakipatikana kwa urahisi, kijakazi aliyefanikiwa kuwaletea wahindi matunda hayo alikuwa akilipwa vizuri. Niliona pengo katika soko hilo na nikazamia kilimo hicho mara moja. Kwa kweli kimenisaidia na ndicho kilinisaidia kuwasomesha wana wangu 14 na bado kinanilipia karo ya baadhi ya wajukuu,” Ogamba anaongeza.

Ekari moja ya shamba lake ameitengea matunda hayo japo amechanganya ndani ya shamba hilo kwenye nafasi zilizoachwa na maparachichi aina ya Hash.

Matunda ya bukini anayolima ni ya rangi ya manjano na anaeleza kuwa kilimo cha matunda hayo si kigumu ikilinganishwa na mimea mingine ambayo anasema huhitaji upaliliaji wa mara kwa mara.

Jinsi ya kufaulu katika upanzi

Yeyote anayewazia kuanza kilimo hicho kulingana na Ogamba, sharti apate mbegu kutoka kwa bukini mbivu. Bukini hizo mbivu hupasuliwa na mbegu zake kuanikwa juani.

“Zikishakauka maji, hupandwa kwa kitalu na baada ya siku kadhaa, zinaota. Kufikia mwezi mmoja hivi, miche ya bukini itakuwa tayari kupelekwa shambani kupandwa,” anaeleza.

Anasema kuwa kabla ya kupanda, ni vyema kutayarisha shamba vizuri kwa kuondoa kwekwe zote. Kisha mashimo yanafaa kuchimbwa nusu futi kwenda chini na mbolea ya samadi au fatalaiza ya kupanda inaweza kutumika.

“Upana kutoka kwa mmea mmoja hadi mwingine uwe mita moja na nusu kwa kuwa bukini zikianza kukua, zinaweka matawi mengi na hivyo ukipanda kwa ukaribu sana, mimea hiyo itakuwa kichaka na ikose kukupa mazao tele,” anashauri.

Ili kuipa nguvu mimea ya bukini na kuifanya isivunjike wakati wa upepo mkali, mzee Ogamba anasema ni vyema kuisimamisha kutumia vijiti na nyaya.

Matunda hayo ya bukini kisha yataanza kuzaa matunda baada ya miezi mitatu. Kadri yanapokomaa, yataanza kugeuka rangi kutoka kijani kibichi na kuwa ya manjano.

Dalili ya tunda lililoiva ni ganda la nje la tunda hilo kuanza kukauka. Matunda hayo yanaweza kuchumwa kwa hadi miaka miwili kabla ya mimea yake kupunguza uzalishaji wake.

Matunda hayo anaeleza mzee huyo yanaweza kuchumwa pamoja na maganda yake au bila na kupelekwa sokoni.

“Ikiwa utavuna kwa kung’oa maganda yanayofunika tunda, lazima uwe na kontena za plastiki kuweka matunda hayo,” anasema.

Hata hivyo, yeye hutumia vifuko vidogo vya neti, vinavyouzwa sokoni. Kila tunda moja huliuza Sh1. Ana wateja kutoka miji ya Kilgoris na Kisii. Kwa mwezi, Omanga anasema hutia kibindoni zaidi ya Sh20,000 kutokana na uuzaji wa matunda hayo.

Vile vile, anaeleza kuwa matunda hayo hayatatizwi na magonjwa ila shida kubwa ambayo amekumbana nayo ni ndege waharibifu wanaokula matunda hayo yanapoanza kuiva na wakati mwingine hulazimika kuwa hapo ili kuwafukuza.

Kulingana na mtaalamu wa lishe Geofrey Nyakundi, matunda ya bukini yana madini mengi ambayo hufaa mwili wa binadamu.

“Gooseberries hazina kalori nyingi na virutubisho vyake husaidia kudhibiti sukari mwilini, kulinda moyo na ubongo ili kuhakikisha viungo hivyo vinafanya kazi inavyostahili,” anasema.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi Malindi wafurika barabarani kusherehekea Aisha Jumwa...

Uhispania wakomoa Ureno ugenini na kutinga nusu-fainali za...

T L