ZARAA: Wakulima washauriwa wafanye vipimo vya udongo

ZARAA: Wakulima washauriwa wafanye vipimo vya udongo

NA SAMMY WAWERU

NI muhimu udongo kufanyiwa ukaguzi na vipimo kujua kiwango cha rutuba iliyomo na cha madini yanayohitajika kuongezwa.

Vipimo vya udongo, kulingana na wataalamu ni miongoni mwa nguzo kuu kufanikisha shughuli za kilimo.

Kabla kuingilia shughuli za kilimo, hususan upanzi mara kwanza katika shamba, mkulima ametakiwa kupima kiwango cha asidi na alikali (pH).

Hatua hiyo itamsaidia kujua madini atakayoongeza kupiga jeki rutuba ya udongo.

“Ni muhimu kutambua kiwango cha virutubisho udongoni. Udongo hujifufua wenyewe ukitunzwa vyema,” amehimiza Sophie Mwaniki, kutoka Crop Nutrition Laboratory Service, maarufu kama Daktari wa Udongo.

Kulingana na afisa huyu, wengi huharibu udongo kwa kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali kuboresha mazao na kukabiliana na kero ya wadudu.

“Iwapo hujui pH wala kiwango cha urutuba cha udongo wa shamba lako, uko gizani kuendeleza zaraa,” Sophie aelezea.

“Unapotambua hali ya udongo wako, itakuwa rahisi kujua fatalaiza, mbolea na dawa unazopaswa kutumia,” afafanua msanidi huyo wa biashara.

Huku wakulima wengi wakijipata kutumia fatalaiza na dawa bila ushauri nasaha wa mtaalamu, Sophie anaonya hatua hiyo ni chocheo la uzalishaji mazao hatari.

Baadhi ya wakulima wakifuatilia mafunzo ya mtaalamu Sophie Mwaniki kuhusu udongo, eneo la Ruiru.  PICHA | SAMMY WAWERU

Anasema ukaguzi na upimaji wa udongo, utasaidia mkulima kuwa na mipangilio bora kupata mazao ya kuridhisha na salama kwa walaji.

Sophie ameiambia Taifa Leo kwamba amepokea malalamishi chungu nzima kutoka kwa wakulima, wakiteta kugharamika kununua fatalaiza kunawirisha mimea na mazao bila mafanikio.

Bei ya fatalaiza ingali ghali licha ya serikali kuzindua mpango wa mbolea ya bei nafuu.

“Mkulima atunze virutubisho vya shamba lake, viumbehai na viumbe wengine wanaosaidia kusawazisha udongo kwa minajili ya mazao bora,” ameshauri.

Shirika analowakilisha, hutoza ada kati ya Sh2, 500 – 5, 000 kupima sampuli ya udongo.

Wakulima wamekuwa wakilalamikia udongo kudhoofika, Sophie akisema changamoto hiyo imechangiwa na matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali.

Aidha, anasisitiza kuokoa hali sharti wakumbatie suala la ukaguzi na upimaji udongo ili kuuboresha.

 

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Kuku na supu ya uyoga

NJENJE: Pakistan sasa yaongoza kwa ununuzi wa bidhaa za...

T L