Bambika

Zari asema hajaingiza mdudu kwa penzi la Mondi na Zuchu

February 27th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

SOSHIOLAITI Zarinah Hassan ambaye wengi humuita Zari Hassan huku mwenyewe akipendelea kujiita Zari the Boss Lady, amepinga uvumi unaoenezwa mitandaoni kuwa sababu kuu ya kuvunjika kwa uhusiano wa Zuchu na Diamond Platnumz ni video yake na bosi wa lebo ya WCB Wasafi wakiwa wameshikana mikono kwa furaha.

Kwenye mahojiano na chombo kimojawapo nchini Tanzania, Zari alikana kuhusika, akidai video hiyo ilipakiwa kuinua wimbo wa baba wa watoto wake.

“Baba T aliniambia video yake haitembei vizuri. Kwamba nimsaidie kwa kuifanyia promo, kisha aipakie, nami nikasema ni sawa. Hapo hapo Zuchu alikuwa amesimama na watoto. Kisha Diamond akaipakia,” alisimulia Zari.

“Yule ni baba wa watoto wangu Tuna mahusiano mazuri na kuna kipindi hatukuwa sawa ila tumeachana nayo na tuko vizuri. Tumekuwa marafiki, tunaweza kupigiana simu kushauriana japo siwezi kurudiana naye,” akaongeza.

Soma Pia: Diamond Platnumz aelekea ‘Zenji’ kumuomba Zuchu msamaha

Pia, alikana madai kwamba ‘Mondi ndiye kawa chanzo cha mpenzi wake na mume wake wa sasa, Shakib Lutaaya, kukasirika na kufuta picha zake kwenye ukurasa wake.

“Mimi na Shakib tumekuwa na matatizo yetu. Nilianza kufuta picha zake kwenye Instagram yangu toka Novemba, Desemba…  Tulikuwa na matatizo makubwa, sasa haiwezi kutokea sasa hivi kuwa Baba T na Zari ndio Shakib anajiweka kwenye hiyo hali kama ya Zuchu. Zuchu kila wiki anaenda na kurudi,” akachekesha.

Msanii Diamond Platnumz (kushoto) na mwenzake Zuhura Othman almaarufu Zuchu. PICHA | MAKTABA

Zari hata hivyo alisema kwamba penzi lake na Shakib bado lipo kwa sana na hakuna chochote kitakacholisambaratisha.

Mama huyo wa watoto watano alisema, Shakib alikuwa na sababu zake za kusafiri.

“Shakib hajaondoka kwa sababu ya video yangu na Diamond, alikuwa ni lazima asafiri ile siku, simlaumu kujisikia jinsi anavyojisikia kwa sababu sikumwambia kuhusu ile video kama ni ya promo. Iwapo nimemvunjia heshima, kutoka moyoni mwangu namuomba msamaha,” akasema Zari, mamake Latifah na Nilan.

Wiki jana baadhi ya mashabiki mitandaoni walifika kwenye ukurasa wake wakitaka kufahamu sababu za Shakib kuonekana na mabegi mengi nchini Uganda. Hata hivyo aliwakemea akitaka wahusike na mambo yao binafsi.