Michezo

Zarika asema ana kiu ya kuvaana na bingwa WBC Yamileth Mercado

May 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MWANABONDIA Fatuma Zarika amesema kwamba bado ana kiu ya kuvaana na bingwa wa sasa wa taji la WBC duniani, Yamileth ‘Yeimi’ Mercado wa Mexico.

Ni matarajio ya Zarika kwamba Yeimi ataridhia kurejea ulingoni kunyanyuana naye kwa mara nyingine licha ya promota wake kusitasita kuyakubali maagano hayo kwenye mchakato ulionanzishwa Januari 2020.

Zarika alimzidi Yeimi maarifa kwa wingi wa alama walipochapana kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 8, 2018 jijini Nairobi. Marudiano yaliyoandaliwa mjini Chihuahua, Mexico mnamo Novemba 16, 2019 yalimshuhudia Yeimi akilipiza kisasi dhidi ya Zarika aliyepokonywa ubingwa huo wa dunia.

Hadi walipomenyana Novemba, Zarika alikuwa ameshikilia taji la WBC kwa kipindi cha miaka minne na kulitetea mara tatu tangu alitie kibindoni kwa mara ya kwanza mnamo 2016.

Japo yalikuwa matarajio ya Zarika kwamba waandalizi wa WBC wangalimpangia kuchapana na Yeimi, bondia huyo wa Mexico alihiari kuvaana na Catherine Phiri wa Zambia chini ya siku 90 katika juhudi za kutetea ubingwa wa taji hilo.

Mchapano kati ya Yeimi na Phiri ulitarajiwa kufanyika nchini Mexico mnamo Machi 2020. Hata hivyo, uliahirishwa kutokana na kanuni mpya zinazodhibiti usafiri katika juhudi za mataifa mengi kukabiliana na maambukizi ya virusi vya homa kali ya corona.

Katika mahojiano yake na gazeti moja la humu nchini, Zarika alisema: “Ni matumaini yangu kwamba vinara wa WBC watabatilisha maamuzi hayo ya awali na kumpangia Yeimi kupigana nami badala ya Phiri. Nahisi kwamba bado sijamalizana na Yeimi ambaye nina fupa kubwa la kuguguna naye.”

Japo anakiri kwamba marejeo yake ulingoni hayatakuwa rahisi, Zarika ameshikilia kwamba atapania kukabiliana vilivyo na ushindani mkali kutoka kwa Yeimi iwapo ombi lake litazingatiwa.

Zarika almaarufu ‘Iron Fist’ alizidiwa maarifa kwa alama 99-91, 98-92 na 99-91 katika mchuano wake wa tatu dhidi ya Yeimi nchini Mexico.

Hadi Serikali ya Nchi za Milki za Kiarabu (UAE) ilipoamrisha kufungwa kwa maeneo yote ya umma kutokana na janga la corona mnamo Machi 15, 2020, Zarika alikuwa akifanya mazoezi katika ukumbi wa Round 10 Gymnasium jijini Dubai.

“Katika mkataba tulioutia saini na Yeimi, kulikuwepo na kifungu cha sisi kurudiana baada ya siku 90 kwa mshindi mpya wa WBC kutetea ubingwa huo. Sidhani kwamba hilo limezingatiwa na wale wanaompangia sasa Yeimi kuvaana na Phiri,” akasema Zarika kwa kusisitiza kwamba atapigania fursa ya kufanikisha pigano dhidi ya Yeimi pindi akaporejea humu nchini kutoka Dubai anakoishi katika nyumba ya kukodi.

Aidha, amefichua azma ya kupunguza uzani zaidi na kuanza kushiriki mapigano ya flyweight ili kuzidisha matumaini ya kutia kibindoni mataji mengine zaidi katika ulingo wa ndondi kabla ya kustaafu.

Anashikilia kwamba atapania kushiriki mapigano ya kitaifa au kimaeneo ya hadi kufikia raundi nane kabla ya kujitosa ulingoni kunyanyuana na mabondia maarufu zaidi duniani.

“Naamini kwamba nitapata washindani kadhaa kutoka Kenya na eneo pana la Afrika Mashariki kabla ya kujitosa katika ulingo wa kimataifa,” akaongeza kwa kusisitiza kuwa hajutii kabisa kushindwa na Yeimi kwa kuwa alipigana naye wakati ambapo hakuna msaada mkubwa aliokuwa akipokezwa na wasimamizi wa masumbwi nchini Kenya.