Michezo

Zarika awakia serikali ya Kenya baada ya kulimwa Mexico

November 17th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Fatuma “Iron Fist” Zarika amepoteza taji lake la dunia la masumbwi kwenye uzani wa kati ya kilo 54 na 55 (Super bantamweight) la WBC na kudai kuwa alifanya hivyo kwa kutaka katika ukumbi wa Poliforo mjini Chihuahua nchini Mexico mapema Jumapili.

Zarika, 34, ambaye alikuwa ameshikilia taji hilo la kifahari tangu avue raia wa Jamaica Alicia Ashley ubingwa kwa wingi wa pointi Oktoba 1, 2016 nchini Marekani, alisalimu amri baada ya Yamileth “Yeimi” Mercado, 21, kulima Mkenya huyo katika pigano hilo la raundi 10.

Majaji walipatia raia huyo wa Mexico ushindi wa alama 99-91, 98-92, 98-92 dhidi ya Zarika, ambaye alikuwa ameshinda mapigano 32 (17 kwa njia ya KO), kupoteza 13 na kutoka sare mechi mbili kabla ya mechi hiyo ya marudiano.

Mercado ameimarisha rekodi yake hadi ushindi 15 (mbili kwa njia ya KO) na vichapo vinne.

Itakumbukwa Zarika alishinda “Yeimi” jijini Nairobi mnamo Septemba 8 mwaka 2018 na kuhifadhi taji lake japo kwa utata kwa sababu mashabiki wengi wakiwemo Wakenya waliamini raia huyo wa Mexico aliibiwa ushindi peupe.

Wakati huo, majaji walimpatia Zarika ushindi wa alama 99-91, 97-93, 94-96.

Mapema mwaka 2019 (mwezi Machi), Wakenya pia waliamini Zarika alichapwa na Mzambia Catherine Phiri jijini Nairobi.

Wengi walisema Zarika alifaulu kudumisha ushindi kwa sababu alipendelewa nyumbani. Baada ya kupigwa mjini Chihuahua, Wakenya waligawanyika kuhusu matokeo hayo.

Baadhi yao walimuonea huruma na kumuunga mkono katika malalamishi dhidi ya serikali. Hata hivyo, sehemu kubwa ya mashabiki ilishangilia ushindi wa Yeimi ikisema Zarika alishindwa kihalali.

Zarika amenukuliwa na runinga ya K24 akisema kuwa “alitupa pigano hilo” kwa sababu “serikali imemtelekeza” na kwamba “hataomba msamaha yeyote kwa kitendo chake.”

“Nataka kuambia mashabiki wangu hakuna mtu yeyote napatia pole, najua kitu ambacho nimefanya na siombi msamaha kwa mtu yeyote. Wakati ambapo nilikuwa napata hiyo ‘belt’, sikuwa na mtu yeyote. Nilikuwa peke yangu.

“Nimekaa na hiyo ‘belt’ miaka nne na hakuna kitu mzuri ishaikuja isipokuwa (usaidizi kutoka kwa kampuni kamari ya SportPesa). Serikali haitaki kushughulika, afadhali mshipi ibaki Mexico, mahali ambapo wataitunza. Wataichunga. Najua serikali yao inawaunga mkono kwa hivyo siombi msamaha mtu yeyote,” alisema baada ya pigano.

Ripoti zinadai kuwa Zarika ameomba mechi ya marudiano dhidi ya Yeimi.