Michezo

Zarika malkia wa magumi mwenye mwili wa chuma

March 11th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

FATUMA Zarika ni miongoni mwa wanabondia wachache wa kike wa humu nchini ambao majina yao yamesalia kutafunwa vinywani mwa mashabiki licha ya viwango vya mchezo huo kushuka pakubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Zarika, 34, alimzidi nguvu mwanamasumbwi Yemileth Mercado wa Mexico mnamo Septemba 2018 na hivyo kutetea kwa mafanikio taji lake la WBC katika kiwango cha super bantamweight.

Baada ya ufanisi huo, mwanandondi huyo ambaye jina lake halisi ni Zarika Njeri Kang’ethe, alifichua azma ya kustaafu katika ulingo wa kurusha makonde mwaka huu.

Safari ya Zarika ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wawili katika mchezo wa ndondi ilianza yapata miaka 19 iliyopita. Anakiri kwamba ugumu wa maisha yake ya utotoni ulichangia pakubwa kufaulu kwake kitaaluma.

Kwa kipindi fulani, Zarika alilazimika kuishi pamoja na mamaye mzazi Aisha, na kakaye mdogo Musa Mohammed, katika chumba kidogo katika mtaa wa Satellite jijini Nairobi. Aisha ambaye ni mzaliwa wa Uganda, alitengana na mumewe Kang’ethe wakati Zarika alipokuwa na umri wa miaka saba pekee.

Musa, 27, kwa sasa ni beki matata wa Harambee Stars na klabu ya Nkana FC nchini Zambia. Mbali na kuiwajibia FK Tirana ya Albania kati ya 2017 na 2018, Musa amewahi pia kuvalia jezi za Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi na washindi mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

“Fatuma ni jina la vichochoroni nililopagazwa katika mtaa wa South B. Nikiangalia nyuma na kutathmini ukubwa wa hatua ambayo nimepiga, hujihisi vyema zaidi. Hakuna kubwa ambalo hunipa tija na fahari kuliko ufanisi wa kuwapa watoto wangu elimu nzuri katika juhudi za kuwaandalia maisha bora,” Zarika aliwahi kusema katika mahojiano yake na kituo kimoja cha runinga humu nchini.

Zarika anakiri kwamba mamaye alikuwa mwepesi wa kumkataza kushiriki ndondi wakati alipokuwa tineja. Mara kwa mara, alionywa vikali na hata kuadhibiwa alipokuwa akifanya mazoezi ya kurusha magumi.

“Kwa mama, mchezo wa ndondi ulikuwa hatari. Asingetaka kabisa kuniona nikijihusisha na masumbwi. Hata hivyo, nilifaulu hatimaye kumwaminisha kwamba ndondi ni sawa na mchezo mwingine wowote,” akasema.

Kwa wakati huo, Zarika alikuwa amesitisha masomo yake katika Shule ya Msingi ya Kabiria, eneo la Dagoretti Kusini, Nairobi. Alikuwa mwepesi wa hasira, mwenye kupenda vurugu na aliyechukizwa na takriban kila kitu maishani.

“Maisha yalikuwa magumu. Magumu zaidi ukifahamu kwamba ungaliamka asubuhi bila kujua lini na wapi cha kutiwa kinywani kingetokea. Haikuwa rahisi kuona mama akijihangaisha sana kulipa kodi ya nyumba na kutulisha,” akasema.

Ili kumpiga jeki mama mzazi, ilimjuzu Zarika kufanya vibarua vya kila sampuli, ikiwemo kazi ya uyaya, angalau walisukume gurudumu la maisha.

Baada ya kupata ujauzito akiwa bado tineja, mshumaa wa matumaini ya Zarika yalining’inizwa zaidi kwenye uzi mwembamba wa imani.

“Maisha yaliyumba. Zaidi kwa sababu sikuwa na elimu wala chochote cha kunipa riziki.”

Akiwa na umri wa miaka 19, Zarika alihamia katika mtaa wa South B, Nairobi kuishi na binamu yake huku akipania kutafuta vibarua vya kumwezesha kujikimu na kuyashughulikia maslahi ya mwanawe Sophia Vuteme aliyezaliwa mnamo Agosti 12, 1997.

Pindi aliposikia kuhusu uwezekano wa kujitosa katika ulingo wa ndondi au soka, Zarika hakusita kujaribu bahati yake katika fani hizo.

“Jirani yetu alinitambulisha kwa rafiki yake ambaye alinipangia kikao na mwanabondia Conjestina Achieng na mwanasoka mmoja. Baada ya kunoa vibaya katika soka, nilihiari kujibwaga rasmi katika ulingo wa masumbwi mnamo 2000 chini ya uelekezi wa Conjestina katika mtaa wa Mathare North,” akaeleza.

Conjestina ndiye mwanandondi wa kwanza wa kike barani Afrika kutia kapuni taji la kimataifa baada ya kumdengua Fiona Tugume wa Uganda katika WIBF Middleweight.

Baada ya kumpiku Mercado kwenye mchapano wa kuwania taji la WBC katika kitengo cha Super Bantamweight, Zarika alikuwa ni mwingi wa matarajio ya kutawazwa Mwanamichezo Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake katika tuzo za SOYA zilizotolewa mwanzoni mwa mwaka huu jijini Mombasa.

Zarika ambaye pia ni mamaye Halima, hata hivyo aliambulia pakavu baada ya kupigwa kumbo na mwanariadha Beatrice Chepkoech ambaye pia alipiku mwanaraga mahiri wa Kenya Lionesses Janet Okello, malkia wa mbio za mita 5,000 katika Jumuiya ya Madola, Hellen Obiri na Celliphine Chespol ambaye ni bingwa wa mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20.