Michezo

Zarika na Phiri nani ni zaidi ya mwingine?

March 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Fatuma ‘Iron Fist’ Zarika ataweka taji lake dunia la WBC la uzani wa ‘Super bantam’ hatarini atakapolimana na Mzambia Catherine Phiri katika mapigano ya SportPesa Nairobi Fight Night ya Jumamosi usiku katika Jumba la mikutano la kimataifa la KICC jijini Nairobi.

Zarika, 34, alitolewa kijasho na Phiri, 32, mnamo Desemba 2, 2017, katika hoteli ya kifahari ya Carnivore kabla ya kumshinda na kuhifadhi taji hili.

Phiri aliwasili jijini Nairobi mnamo Machi 19 tayari kwa pigano hili litakalopeperushwa katika runinga kadhaa za Kenya ikiwemo NTV.

Fatuma ‘Iron Fist’ Zarika (kushoto) na Catherine Phiri walipohutubia wanahabari Machi 22, 2019, jijini Nairobi. Picha/ Jeff Angote

Pigano hili litakuwa la Zarika la 45. Ameshinda mapigano 31 yakiwemo sita yaliyopita na kupoteza 12 pamoja na kutoka sare mara tatu. Naye Phiri anajivunia ushindi mara 16 ikiwemo mapambano matatu yaliyopita na kupoteza mapigano mara tatu.

Promota wa mapigano haya yatakayosimamiwa na refa Thabo Spampool na majaji Michael Neequaye, Fillemon Mweya na Irene Semakula ni Thomas Kiswili kutoka Afribox Camp International.

Tiketi za kawaida ni Sh1000, huku wageni mashuhuri wakilipia Sh3,000 kuingia katika ukumbi utakaotumika kwa pigano hili katika jumba la KICC.

Ratiba (Machi 23, 2019):

Pigano la kwanza (uzani wa Super Light – raundi sita) – Nicholas Mwangi (Kenya) na Idd Mkwera (Tanzania)

Pigano la pili (Uzani wa Super Light – raundi sita) – Sarah Achieng’ (Kenya) na Joice Awino (Kenya)

Pigano la tatu (uzani wa kati – raundi nane) – Rayton Okwiri (Kenya) na Pascal Bruno (Tanzania)

Pigano la nne (uzani wa Super Welter – raundi nane) – Hassan Mwakinyo (Tanzania) na Sergio Gonzalez (Argentina)

Pigano la tano (taji la dunia uzani wa Super bantam – raundi 10) – Fatuma Zarika na Catherine Phiri